Friday, July 19

Siri ya miaka 100 ya mke wa Chifu Makongoro

0


Dodoma. Wahenga walisema, kuishi kwingi ni kuona mengi pia wakasema wakiwaelezea watu walioishi umri mrefu kwamba wamekula chumvi nyingi.

Kwa kuwa wameona mengi, baadhi ya watu hutamani kwenda kujifunza kutoka kwao na kuitathmani dunia ya leo kwa mtazamo wa zamani.

Miongoni mwao ni Munuli Makongoro ambaye umri wake unakadiriwa kuwa miaka 100 na jambo la kufurahisha kwake ni kwamba bado yu mwenye afya njema, anasikia vizuri, anaona sawasawa na ana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo ya sasa na ya kale.

Huyu ni mke wa 27 kati ya 47 wa aliyekuwa Chifu wa Nyamuso (Bunda), Makongoro ambaye anaelezwa kwamba alikuwa na msimamo mkali.

Anakadiriwa kuwa alizaliwa mwaka 1918 katika Kijiji cha Nyamuswa akitokea kwenye familia ya watoto watano kwa baba yake aliyekuwa na familia ya kawaida.

Anasema alichumbiwa na Chifu Makongoro akiwa na miaka 18 na alikubali kuolewa kwa heshima ya kuingia katika familia ya kichifu na baadaye waliongezeka wengine 20 waliofanya idadi ya wake wa Chifu kufikia 47.

Bibi huyu ana simulizi ndefu zinazovutia lakini kubwa ni jinsi walivyoishi kwa umoja, upendo na mshikamano kiasi cha kujenga nyumba kwa pamoja. Fikiria maisha ya sasa ya uke wenza kwa baadhi ya familia.

“Mimi sikuolewa kwa kulazimishwa. Nilikuwa nyumbani halafu nikaja kuchumbiwa na nilikubali mwenyewe kwani ilikuwa ni heshima kuingia katika familia ya kichifu,” anasema Munuli ambaye wiki iliyopita alitembelea Bunge jijini Dodoma.

Anasema hata baada ya kifo cha Chifu Makongoro mwaka 1958, maisha ya familia hiyo yameendelea kujaa umoja na mshikamano, wakipendana na kuguswa na matatizo ya kila mmoja wao. Anasisitiza, “Hakuna anayeweza kuwa na furaha ikiwa kwa mwenzake kuna huzuni.”

Anasema enzi za uhai wa mume wao, walikuwa wanalima na kuunganisha mazao yao pamoja. Anakumbuka jinsi walivyokuwa wanalima pamba na katani kwa wingi kiasi cha kufanikiwa kununua matrekta na magari huku wakiongeza mifugo kila mwaka.

“Hata alipokufa marehemu mume wetu, sisi tuliendelea kama kawaida kufanya kazi kwa umoja na ndiyo maana alituachia nyumba ikiwa haijaisha lakini (Baba wa Taifa) Mwalimu Nyerere alikuja kutushauri tukaunganisha nguvu zetu tukaimalizia pale Musoma Mjini. Kwa ujumla hatujawahi kugombana sisi kwa sisi,” anasema.

“Wenzetu wengine wametangulia mbele ya haki, tumewazika na kuwalilia na sisi 10 tuliobaki bado tunaendelea na umoja wetu na kusaidiana ingawa baadhi ya watoto wanaanza kutugawa.”

Siri ya maisha marefu

Moja ya chakula anachokisifia kusaidia kurefusha maisha yake na wenza wake, ni ugali wa muhogo na ulezi, lakini si hayo tu, pamoja na kujiepusha na mambo ya anasa ambayo yaliwaepusha na magonjwa.

Munuli ambaye mumewe alifariki miaka 60 iliyopita akimwacha na watoto watatu, anasema maisha ya wakati huo huwezi kuyalinganisha na ya sasa. Anasema siku hizi kumejaa dharau, kiburi na kutojali hali ambayo anaamini kwamba inachangia watu wengi kufariki dunia wakiwa na umri mdogo.

Kwake anasema heshima ilikuwa ni sehemu ya ibada. Kila wakati alilazimika kufikiri namna anavyoweza kuishi maisha yasiyokuwa na lawama au kunyooshewa kidole akiwa mke wa chifu.

Anasema ilikuwa ni desturi na utamaduni kwao kujipambanua kwa vitendo vyema kwa kuwa walikuwa wake wa mtu muhimu kwa jamii na kielelezo cha utawala wao.

Hakuna kusambaratika

Tangu mwaka 1958 walipoanza maisha mapya bila ya Chifu Makongoro, bibi Munuli anasema wameendelea na maisha ya ujamaa na kushikamana zaidi ili kuwatunza watoto wao na kuendeleza mali walizoachiwa.

“Wakati anakufa alikuwa amejenga shule, alijenga kituo cha afya kwa ajili yetu, akajenga ofisi na sasa bado zinafanya kazi.”

“Lakini alituachia nyumba mjini Musoma ambayo ilikuwa haijaisha na sisi tukafanya kikao chini ya mke mkubwa tukaenda kuimalizia na ndiyo iliyosomesha watoto wote hadi vyuoni,” anasema.

Tofauti ya maisha

Anaona kuna tofauti kubwa ya maisha ya sasa na yale ya zamani. Anasema hivi sasa kuna dharau, matusi, hali ya kutojali wakubwa na mavazi mambo ambayo yanawaondolea sifa mabinti wengi na vijana hata kuonekana ni watu wa mtaani.

“Tena hawafanyi kazi kama tulizokuwa tunafanya sisi, wanakula vyakula vya ajabu, hawana heshima kwa wakubwa, hawana huruma kwa wenzao na sijui hali hii kama inaweza kuwafikisha katika mahali sahihi,” anasema.

Kwa nini hawakuolewa

Kwa kawaida wajane wengi huolewa baada ya kupoteza waume, lakini hilo halikutokea kwa wake wa Chifu Makongoro. Munula anasema licha ya wengi wao kuachwa wakiwa na umri wa unaofaa kuolewa, waliamua kubaki nyumbani kulinda heshima ya chifu ingawa. Hata hivyo, anasema wako watoto wengi waliozaliwa na watu wengine lakini kwa mila yao waliitwa ni watoto wa Chifu.

Kama mmoja wao angeamua kuolewa na mume mwingine, ingempasa kuondoka na kwenda kuanza maisha yake na kutengwa na jamii na isingekuwa rahisi kuondoka na watoto wa na kuwapeleka katika ukoo mwingine.

Mjukuu wa Makongoro ambaye ni wakili Abdala Makongoro anasema kifo cha babu yao hakikujulikana na kila wanapotaka kujua ukweli halisi huwa kunajitokeza chenga ambazo hadi leo hawajui sababu zake.

Makongoro anasema hofu ya kifo hicho haikuwa kwa watu wachache tu bali ilijengeka tangu muda mrefu na hata familia yao ilianza kutilia mashaka lakini walimuachia Mungu.

Kwa sasa waliosalia hai miongoni mwa wake wa Chifu Makongoro ni 10 ambao bado wanaishi kwa upendo.

Share.

About Author

Leave A Reply