Thursday, August 22

Siri ya Chuji, Boban kutikisa soka la Bongo hii hapa

0


By Olipa Assa

KWA mwonekano wa staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Athuman Idd ‘Chuji’ unaweza ukamchukulia ni mchezaji anayejisikia, asiye na ushirikiano.

Hata hivyo, mwenyewe anadai hayuko hivyo na kukiri yeye pamoja na kiungo wa Yanga, Haruna Moshi ‘Boban’ wanachukuliwa ni wachezaji waliopinda bila kujua nini kipo nyuma ya pazia kinachowafanya wasiwe watu wa kujichanganya na mashabiki wa soka.

“Soka la Tanzania lina changamoto nyingi, napenda mpira upo kwenye damu, shida inakuja kwa baadhi ya watu ambao wanapenda kuchanganya unafiki na jasho ambalo nalitoa uwanjani, nilipogundua hilo niliamua kuchagua mfumo wangu wa maisha.

“Kama kuna watu wanaozungumziwa kuwa na kiburi, kujisikia, ukimya, makauzu yaani majina yote kwenye soka la Tanzania ni mimi na Boban ambao hatuna maneno maneno na watu wala mashabiki.

“Kiukweli bado tuna nguvu ya kucheza soka na ndio maana tunapotea halafu watu wanashangaa tumerejea tena wanaanza kusema hawa watu wapo, bora uwe rafiki wa wasukuma mikokoteni kuliko kuwa karibu na watu ambao wanainafikia kazi yako, hilo limewakatisha tamaa watu wengi na kujikuta wakiacha soka mapema sana,” alisema.

Kwa upande wa Boban, aliwahi kuzungumzia alivyopenda kujichanganya na watu wa soka kipaji chake hapendi kiingizwe siasa ambazo zitamfanya ajisikie anafanya kazi isio na thamani.

“Ninavyolichukulia soka, tofauti sana na wale ambao wanapenda kuingiza siasa, huo mpira unachezwa uwanjani lakini utakuta maneno maneno, hilo ndilo linalonifanya niwe nanyamaza na kufanya maisha yangu ambayo yananiweka huru,” alisema.

Chuji aliwatolea mfano viungo wa Simba, Jonas Mkude na Said Ndemla wakiwatema wanaanza kuwaita wazee, wakati wanaweza kucheza miaka 10 mbele, alienda mbali zaidi kwa kumzungumzia Meddie Kagere mwenye mabao 22 mpaka sasa.

“Tanzania tunachukuliana poa sana, Kagere na sisi tuna tofauti gani kiumri au kwa kuwa ametoka nje ya mipaka yetu anaonekana kijana wa miaka 28, lakini unaona anavyofanya kazi yake kwa ubora kuna misingi aliyopitia kwenye mpira. “Mfano mimi nimecheza ligi madaraja yote kwa maana ya daraja la nne, tatu, pili la kwanza kisha Ligi Kuu, hatua hizo zimenifunza mengi ambayo siyumbishwi kisoka kwani nimecheza mifumo yote, najilinda kiwango, natunza mwili wangu, soka naliheshimu linaniheshimu, hata Kagere soka analiheshimu linamheshimu na ndio maana anawaweka benchi chipukizi,” .

Alipoulizwa kama soka limemlipa au la! Alijibu “Kanuni ya maisha yangu na hata ninachowashauri wadogo zangu ni ukipata 10 tumia mbili, weka nane kwa akiba ya maisha yako, kwa hilo Alhamdulillah, nilijua kutunza kidogo nilichokuwa napata, hivyo siwezi kujutia chochote.”

Anasema kama kuna vijana ambao wanapenda kujifunza mpaka kesho kutoka kwake ni Simon Msuva (Difaa Hassan El Jadid) na Himid Mao (Petrojet ya Misri) ambao wamekuwa wakimpigia simu mara kwa mara kutaka kuelekezwa baadhi ya vitu muhimu vya soka.

Alisema kitendo cha Mbwana Samatta (Genk, Ubeligiji) na staa wa muziki wa Bongo Fleva, Ali Kiba kuanzisha mechi ya hisani inayolenga kuisaidia jamii, alishauri kiigwe hata na wanasiasa.

“Ndio maana tunakubali kucheza ili kuunga mkono juhudi zao, sio kitu kibaya wanasiasa kuiga mfano huo, warudishe shukrani kwa wale ambao wanaowaongoza,” alisema.

Mbali na hilo alizungumzia ligi ya msimu huu ipo vizuri kwa maana imeisha kwa ushindani akidai tofauti ya pointi za ubingwa ni ndogo. “Kuelekea mwisho wa msimu, Simba na Yanga zimetoana jasho hilo lilikuwa jambo zuri, pia kuna timu ambazo zimefanana pointi, hii inaleta changamoto ya upambanaji,” alisema.


Share.

About Author

Leave A Reply