Saturday, July 20

SIMULIZI ZA MUZIKI NA ANKO KITIME: Tasnia ya burudani ni kama bustani

0


Moja ya mambo ambayo ni mara chache utayasikia ni viongozi wa nchi hii kuongelea mchango wa tasnia ya burudani katika pato na ustawi wa jamii wa Taifa letu.

Katika maongezi yangu na mchumi mmoja aliyewahi kuwa mshauri wa ngazi ya juu wa mambo ya uchumi Tanzania, alionyesha kushangaa nilipomwambia kuwa kuna ripoti inaonyesha kuwa mwaka 2012 tasnia ya ubunifu ilipata Sh640 bilioni kwa mujibu wa ripoti ya The Economic Contribution of Copyright-Based Industries in Tanzania.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa tasnia hii iliajiri watu wengi zaidi kuliko madini, afya, ujenzi, usafirishaji na mawasiliano. Takwimu hizi siyo za ajabu kwani picha ya namna hii inajirudia katika nchi nyingine pia.

Lakini katika nchi nyingine Serikali zimeweka mazingira bora ya kuendeleza tasnia hii ili kupata faida zote zitokanazo na uimara wake.

Katika ripoti mpya iliyotayarishwa na kampuni maarufu ya Pricewaterhouse Coopers SA ya Entertainment and media outlook: 2017 – 2021 An African perspective ambayo imeziangalia nchi za Nigeria, Afrika ya Kusini, Kenya, Ghana na Tanzania kwa mara nyingine tena inaonyesha jinsi tasnia hii ilivyo na uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya nchi.

Pamoja na kuingiza kipato kwenye mifuko ya wananchi na pato la Taifa, tasnia ya burudani ni muhimu kwa jamii.

Burudani huleta furaha, hupunguza msongo wa mawazo na hivyo kuleta amani katika jamii.

Burudani pia huondoa uchovu baada ya kazi na huhamasisha utendaji zaidi wa kazi, na husahaulisha machungu na matatizo, burudani pia hutumika kuelimisha, kujenga maadili na hata kujenga umoja wa kitaifa.

Kwa upande mwingine katika mazingira ya kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, ni muhimu kuelewa kuwa baada ya kazi lazima kuwepo na burudani yakujipongeza kwa kazi nzuri, na kuondoa uchovu na pia kutia motisha ya kufanya kazi zaidi ili kupata kipato cha kuweza kugharamia burudani, na hapo ndipo Serikali nayo inapata nafasi ya kukusanya kodi.

Nimeshawahi kueleza katika moja ya makala zangu za nyuma jinsi wakoloni walivyohakikisha kuwa wanatenga sehemu za burudani na hivyo karibu kila makao makuu ya wilaya kukawa na ukumbi uliojulikana kwa jina la community center.

Pia, kulitengwa sehemu za burudani kwa watoto, ambapo Serikali wakati huo iliwajengea ‘bembea’ na vifaa vingine vya kuchezea, pia karibu kila mji mkubwa ulikuwa na japo na jumba moja la sinema na maeneo mengi ya wazi kwa ajili ya michezo mbalimbali kama soka, mpira wa pete, mpira wa wavu na kadhalika.

Na baada ya Uhuru, umoja wa vijana wa chama cha Tanu ulihakikisha kuwa vijana wake wana sehemu za burudani karibu kila mji, na miji mingi ilikuja kuwa na maeneo yaliyoitwa vijana social halls, katika social halls hizi vijana walikutana kwa ajili ya burudani, wakafahamiana, na hata kuwa sehemu muhimu ya kujenga chama chao, kumbi hizi siku hizi nazo zinelekea kupotea kabisa kwa kubadilishwa matumizi.

Kutengeneza ‘fremu’ za maduka ndio ubunifu mkubwa ulipogota wa kuongeza kipato.

Siyo siri kuwa kuna uhaba mkubwa wa sehemu za kufanyia shughuli za burudani kutokana na community centers karibu zote kama ilivyo kwa social halls zilizotajwa kugeuzwa matumizi na hivyo miji mingi haina sehemu za burudani zaidi ya kuwa na viwanja vya mpira na mara nyingi viwanja hivi ni vya shule na sio viwanja vilivyotengwa kwamakusudi hiyo na miji.

Kwa kuona tatizo hili nilifunga safari mpaka Chuo Kikuu cha Ardhi kwani huko ndiko wanakotoka wataalamu wa kupanga miji.

Nilimuuliza profesa mmoja kutoka chuo hicho, kwa nini wanachuo wanaotoka hapo hawatengenezi ramani za miji zenye sehemu za burudani, hata katika ramani za miji mipya sehemu hizo zinakosekana.

Jibu lake lilinishangaza. Profesa aliniambia kuwa wanafunzi wanafundishwa umuhimu wa kuwepo kwa sehemu za burudani katika miji, na katika ramani zao sehemu hizo huwekwa, lakini maamuzi ya kisiasa hubadili matumizi ya sehemu hizo.

Profesa huyo alinigusia kuhusu mkutano wa wachora ramani uliokuwa umefanyika Afrika ya Kusini siku chache zilizopita ambapo umuhumu wa nafasi hizo katika jamii ulisisitizwa.

Nasisitiza tena kuwa tasnia ya burudani ina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii. Mchango kutokana na kuwa ni tasnia ambayo ikipangwa vyema ni chanzo kikubwa cha pato la Taifa kwa fedha za ndani na za kigeni, na ni sehemu muhimu ya kujenga Taifa lenye furaha

Share.

About Author

Leave A Reply