Saturday, August 24

Simba yatwaa ubingwa kwa kishindo Uwanja wa Namfua

0


By Olipa Assa

Dar es Salaam. Simba imetetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwafunga Singida United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Singida.

Simba imetwaa ubingwa huo baada ya washambuliaji wake nyota Meddie Kagere na John Bocco kila moja kufunga bao moja katika kila kipindi katika mchezo huo.

Simba ilianza kupata bao dakika ya 10 kupitia kwa Kagere akiunganisha krosi ya Mohammed Hussen ‘Tshabalala’ iliyoshindwa kuokolewa na beki wa Singida United, Salum Kipaga na kumkuta Kagere hakufanya makosa kwa kupiga shuti lililomshinda kipa Said Lubawa na kujaa wavuni.

Bocco alifunga bao la pili dakika 64, akiunganisha krosi ya Emmanuel Okwi akiwa yeye na goli baada ya kipa wa Singida, Lubawa kuumia na kutoka nje na kutoa mwanya kwa nahodha wa Simba kufunga bao hilo.

Kiufundi wachezaji wa timu zote walishindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na Uwanja wa Namfua kukosa ubora na mipira ilikuwa inashindwa kutulia badala yake ilikuwa inadunda dunda.

Hata bao walilofungwa Singida United dakika ya 10, Kagere alitumia akili ya ziada kutozubaa kutumia nafasi kutokana na beki Kipaga kushindwa kuokoa kwa ufundi alipokuwa anataka kuutuliza chini ndipo ukamponyoka.

Simba, imezoeleka kucheza mpira wa pasi nyingi na za chini chini, lakini hilo lilikuwa gumu kutokana na uwanja kutokuwa rafiki kwao ingawa kwa sehemu walifanikiwa kumiliki kipira.

Mara nyingi pasi zilikuwa zikipigwa hazifiki sehemu sahihi kwani wachezaji walikuwa wanabutua butua ili mladi liende.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alitumia mfumo wa 3-4-3 mbele alimuweka John Bocco (9),Kagere (10) na Okwi (11), eneo la kati liliongozwa na Kotei, Niyonzima na Mzamiru, upande wa mabeki ni Gyan,Tshabalala,Mlipili na Nyoni.

Kipindi cha pili Simba iliingia kwa kushambulia ambapo waliwakosa kosa Singida United mpaka dakika 64 ambapo Bocco alifunga wakati kipa Lubawa akiwa nje ya uwanjani.

Katika harakati za kuokoa Lubawa aliteleza mpaka nje ya uwanja ambapo aliumia wakati ananyosha mkono, mwamuzi hakuona ndipo Bocco akafunga bao la pili, hivyo Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Kocha Aussems alifanya mabadiliko dakika ya 75 aliamua kumtoa mshambuliaji Okwi akamuingiza kiungo mkabaji Jonas Mkude. 

Kikosi cha Simba kiliongozwa na Deogratias Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.

Waliokuwa benchi ni alikuwa Aishi Manula, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Adam Salamba na Rashid Juma.

Kikosi cha Singida United ni Said Lubawa, Frank Zakari, Gilbert Mwale, Salum Kipaga, Kenned Wilson, Rajab Zahir, Borniface Maganga, Issa Makamba, Jonathan Daka, Habib Kiyombo na Geofrey Bahati Mwashiuya.

Share.

About Author

Leave A Reply