Sunday, August 18

Simba yaipora Yanga taji kama utani vile

0


By Olipa Assa

Dar es Salaam. Yanga wanatetemeka na sasa ni dhahiri Simba wanautaka ubingwa wao kwa mara nyingine tena msimu huu. Kasi yake ya kutafuna viporo imezidi kuwa tishio kwa watani zao hao ambao wameketi kileleni kwa muda mrefu.

Licha ya kuwa eneo gumu la kukusanya pointi Ligi Kuu Bara, lakini Simba imehimili vishindo na kukusanya alama tisa kwenye michezo minne iliyokipiga Kanda ya Ziwa, ikipoteza mbele ya Kagera Sugar kwa kuchapwa mabao 2-1.

Imeshinda mechi tatu dhidi ya Alliance FC, KMC na jana imevuna alama zingine tatu nyumbani kwa Biashara United pale mjini Musoma, ambako kunaaminika ni machinjio hatari msimu huu.

Ushindi mbele ya jeshi la Kocha Amri Said kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, umeifanya Simba kufikisha pointi 69 ikiwa ni pointi tano nyuma ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga wenye alama 74.

Pia, Simba ina mechi tano mkononi ili kulingana na Yanga iliyocheza mechi 32 mpaka sasa dhidi ya mechi 27 za Simba. Hesabu za ubingwa wa Simba msimu huu kwa sasa ziko wazi kabisa.

Kwa hesabu za vidole tu, Simba wako kwenye nafasi nzuri ya kubeba ndoo kwa mara nyingine msimu huu.

Iko hivi. Kama Simba itapata ushindi kwenye mechi zake tano za viporo itavuna alama 15 ambazo zitaifanya kufikisha pointi 84 wakati Yanga itabaki na alama zake 74 huku zote zikiwa na mechi 32 na kubakiwa na tano za kumaliza msimu.

Kwa hesabu za haraka haraka, Simba inahitaji kupata ushindi kwenye mechi nane tu kati ya mechi 11 ambazo zimebaki kabla ya kumaliza ligi.

Yaani kama itashinda mechi zake zote itafikisha alama 93 huku Yanga nayo ikishinda mechi zake itavuna alama 83.

Kwa maana hiyo Simba ambayo inaendelea kutafuna viporo vyake inahitaji dakika 720 ambazo ni sawa na mechi nane kusaka ubingwa. Katika mchezo wa jana, ikicheza mbele ya mashabiki lukuki walioujaza uwanja huo, ilianza kwa kasi huku nahodha wake John Bocco akiongoza shughuli ya mauaji kwa vijana wa Saidi.

Ilimchukua Bocco dakika 33 kuitanguliza Simba kwa kupachika bao maridadi la shuti kali la mguu wa kushoto ambalo liligonga mwamba na kuzamia upande mwingine huku kipa wa Biashara United, Nourdine Balora akiruka bila mafanikio.

Balora raia wa Burkina Faso, hakuwa ameruhusu wavu wake kuguswa kwenye mechi tano mfululizo, lakini jana Bocco akachafua kwa kumtungua.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha shangwe za mashabiki wa Simba, lakini hakukuwashtua Biashara United ambao, walikuwa wakicheza soka safi na kujaribu kupandisha mashambulizi kusaka bao la kusawazisha.

Hata hivyo, wakati Biashara wakijaribu kupandisha mashambulizi, dakika ya 40 Asante Kwasi, ambaye alianza kwenye mchezo huo kabla ya kumpisha Yusuph Mlipili dakika ya 84, alichonga krosi matata iliyotua kwenye kichwa cha Bocco na kuihakikisha Simba ushindi wa mabao 2-0 hadi mapumziko.

Hata hivyo, mabeki wa Biashara United itabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kumlinda vyema Bocco, ambaye jana alikuwa mwiba. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu. Biashara waliendelea kucheza soka la kutulia, lakini safu yake ya ushambuliaji haikuweza kuupenya ukuta wa Simba ulioongozwa na Juuko Murshid, Kwasi, Nicholas Gyan na Paul Bukaba uliokuwa makini kumlinda kipa Deogratias Munish (Dida).

Katika kusaka matokeo timu zote zilifanya mabadiliko na dakika 58 Bocco alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere, ambaye hata hivyo hakuweza kutanua rekodi yake ya mabao baada ya kushindwa kutikisa nyavu.

Kwa upande wa Biashara United alitoka Waziri Junior na nafasi yake kuchukuliwa Tariq Seif dakika ya 54 ya mchezo. Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuweza kubadili matokeo kwani hadi kipyenga cha mwisho Simba ilitoka na ushindi wa mabao 2-0

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema mchezo huo ulikuwa nafasi nzuri kwa washambuliaji wa Simba kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuwania kiatu cha dhahabu.

Kwa sasa Kagere ndiye kinara wa mabao akitupia mara 16 sawa na Salim Aiyee wa Mwadui huku Heritier Makambo wa Yanga akiwa na mabao 15 na Bocco mwenye mabao 14 baada ya jana kutupia mawili.

“Bocco anazidi kumsogelea Makambo ambaye ana mabao 15, amefikisha mabao 14 kutoka 12 aliyokuwa nayo awali. Sasa sio huyo tu, Okwi naye anakuja kasi kutoka mabao saba na sasa amefikisha 10, huu ni ushindani wa aina yake,” alisema.

Kipa namba mbili wa Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’ jana alianza kwenye mchezo huo akimpumzisha kipa namba moja, Aishi Manula.

Kocha wa zamani wa makipa wa Simba, Idd Pazi alisema kwenye mchezo huo, Dida alionyesha kiwango kizuri na kama atacheza mechi tano mfululizo basi atarudi katika ubora wake.

“Dida sio kipa mbaya kitendo cha kutokucheza mara kwa mara kinamtoa mchezoni na ile ari ya kujiamini, ndio maana nafasi ya mlinda mlango inakuwa ngumu kwa kocha kumbadilisha ovyo,” alisema.

Kiungo wa kimataifa wa Simba, Haruna Niyonzima atakosa mechi mbili dhidi ya Prisons na Mbeya City baada ya kulimwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo kutokana na kadi mbili za njano kwa mchezo mbaya alioonyesha dhidi ya wachezaji wa Biashara.

Share.

About Author

Leave A Reply