Sunday, August 25

Simba tema mate chini mzuka wampanda Aussems kinoma

0


INAINGIA siku ya nne tangu Simba itue Sauzi kupiga kambi ya mazoezi, lakini unaambiwa licha ya hali ya hewa kuwa ya baridi, hiyo haijawazuia nyota wa timu hiyo kutimiza wajibu wao mbele ya Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems kwani wote wanafurahia mazingira.
Simba imeweka kambi katika Mji wa Rustenburg ndani ya hoteli ya The Royal Marang ambayo inajitosheleza kwa kila kitu, pia mkumbuke hoteli hiyo ndipo walipokaa nyota wa timu ya Taifa ya England ilipokwenda kushiriki Kombe la Dunia 2010.
Baadhi ya nyota wa klabu hiyo wamedai wanafurahia mazingira huku wakila dozi za Kocha Aussems anayehesabu siku za kuja kuanza ngarambe ya Ligi Kuu Bara na michuano mingine ya msimu wa 2019-2020 ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nyota hao wanaeleza kambi yao ina kila kitu ikiwamo mahitaji ya viwanja vya mazoezi, gym, sauna, sehemu ya chakula kinapatikana ndani ya eneo la hoteli, hakuna haja ya kukwea mabasi kutoka nje na kwa ajili ya kutafuta mahitaji hayo.
Hali hiyo imewapunguzia usumbufu na kuongeza morali ya kufanya kazi kwa nguvu kuhakikisha watakaporudi Dar es Salaam kwa ajili ya Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano mengine ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika wawe moto ni mabao kwenda mbele.
Tayari Kocha Aussems amekuwa akiwapigisha tizi la maana vijana wake ndani na nje ya uwanja kwa nia ya kuwajengea uimara utakaowasaidia kwenye michuano watakayoshiriki, ili ikiwezekana wafike mbali zaidi ya mambo waliyofanya msimu uliopita walipotetea taji la Ligi Kuu Bara na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iking’olewa na TP Mazembe ya DR Congo.

BARIDI KAMA KAWA
Hata hivyo, hali ya hewa ya nchini Afrika Kusini kwa sasa ni baridi kidogo jambo linalowafanya baadhi ya watu wanapokuwa nje kwa ajili ya shughuli zao kuvalia nguo nzito kama masweta na majaketi.
Hali hiyo kwa jana Jumatano katika mji wa Rustenburg ambako Simba wamejificha hali ilikuwa nyuzi joto 20 na jua, huku jiji la Johannesburg likiwa na 17, ambayo ni tofauti na Dar es Salaam.
Hali ya hewa ya Dar es Salaam jana Jumatano ilikuwa nyuzi joto 29 jua, mawingu na mvua ndogo.
“Huku kila kitu kinakwenda vizuri kuna hali ya utulivu kilichopo ni mazoezi, kula na kupumzika,” alisema mmoja wa watu walio kwenye msafara huo.
Hata hivyo, nyota wanne waliokuwa wamebaki Dar es Salaam waliondoka jana Jumatano kwenda kuungana na wenzao. Wachezaji hao ni Mkenya Francis Kahata, Mnyarwanda Meddie Kagere, Msudan Shiboub Sharaf na Mkongo Deo Kanda.

NAMBA ZA MOTO
Kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam Kocha Aussems alisisitiza anataka kutumia wiki mbili za kambi yao kuwasoma vijana wake, sambamba na kuwapima kwenye mechi tatu kisha kuja kuliamsha kwenye Simba Day, lakini tayari kuna vita mpya imezuka kikosini.
Inaelezwa kwa sasa kuna vita kubwa kwenye nafasi tatu ndani ya kikosi hicho, kuanzia kwenye ukipa, beki ya kushoto na eneo la kiungo mshambuliaji.
Ukiacha vita ya safu ya ushambuliaji yenye Mkenya Francis Kahata, Mnyarwanda Meddie Kagere, Mkongo Deo Kanda, Mbrazil Wilker Henrique Da Siver na Mzawa John Bocco, kule kwenye safu ya ulinzi ndio kuna balaa zaidi na linaanzia kwa makipa, Beno Kakolanya na Aishi Manula ambao wote kwa pamoja viwango vyao si mchezo.
Kakolanya ambaye amesajili akitokea Yanga baada ya kuvunja mkataba, ni miongoni mwa makipa wanaotegemewa Taifa Stars kutokana na kufanya kwake vizuri ingawa hakuwepo kwenye AFCON kutokana na kushindwa kwenda sawa na mabosi wake wa Jangwani.
Sasa anavaana na Manula anayejulikana kama ‘Tanzania One’ kutokana na kiwango anachokionyesha Simba na Taifa Stars.
Makipa hawa walikaririwa kila mmoja akisema, wapo hapo kwa lengo la kuisaidia Simba ifikie malengo, lakini wao wakifunguka hivyo, shughuli ipo beki ya kushoto ya Gadiel Michael na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambao wote wamo kikosi cha Taifa Stars.
Tshabalala ndiye alikuwa tegemeo la Simba kabla ya Gadiel kutua msimu huu akitokea Yanga lakini naye ni tegemeo la Stars na alicheza mechi idadi kubwa ya mechi za Afcon.
Ushindani mwingine upo pale mbele namba 10 ambako kuna Hassan Dilunga na Ibrahim Ajibu ambao wanafanana staili ya uchezaji.
“Nimerudi kwenye timu, ninachoomba tuwe wamoja,” alisema Ajibu.

Share.

About Author

Leave A Reply