Thursday, August 22

Simba, KMC afe kipa afe beki lazima mtu aumie Kirumba

0


By Saddam Sadick

Mwanza. Baada ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata dhidi Alliance FC jana, mabingwa watetezi Simba watashuka uwanjani kesho Alhamisi kuwavaa KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Simba imeshacheza mechi mbili Kanda ya Ziwa imeshinda mmoja na kupoteza mmoja na kesho watacheza mechi ya tatu dhidi ya KMC.

Simba iliyocheza mechi 25 wamekusanya pointi 63 wanahitaji alama tatu ili kuendelea kuwasogelea wapinzani wao Yanga, wanaoogoza Ligi kwa pointi 74 baada ya kucheza michezo 32.

Mchezo baina ya KMC na Simba unatarajia kuwa ushindani kutokana na kila upande kuhitaji ushindi ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alisema pamoja na ratiba kuwawia ngumu, lakini mkakati wao ni kuendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo wanavuna pointi tatu.

Kocha huyo alisema kutokana na hali ilivyo, kwa sasa atakuwa akiwapanga wachezaji tofauti huku wengine wakipumzika ili kufikia malengo yao ya kutetea ubingwa wao.

“Ratiba ni kama unavyoiona ni ngumu kweli, lakini hatuna namna tutaendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo tunatafuta pointi tatu bila kuchoka,” alisema Aussems.

Kocha huyo aliongeza anaamini mchezo wa leo hautakuwa rahisi kutokana na ushindani walionao wapinzani wao na kwamba dakika 90 ndizo zitaamua.

Wakati Simba wakitamba hivyo, Meneja wa KMC, Faraji Muya alisema kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo.

Alisema wachezaji walio katika mpango wa kocha wako vizuri kisaikolojia na morari hivyo pointi tatu ni muhimu katika harakati zao za kujiweka nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.

“Kwa ujumla maandalizi yapo vizuri tofauti na wachezaji waliokuwa majeruhi wengine wana ari nzuri tunaenda kupambana lakini tunajua mchezo utakuwa mgumu,” alisema Muya.

Share.

About Author

Leave A Reply