Sunday, August 18

Shirika lashauri mtaala somo la ulinzi wa mtoto

0


By Nazael Mkiramweni, Mwananchi

Dodoma. Shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania limeishauri Serikali kuangalia namna ya kuweka somo la ulinzi wa mtoto kwenye mitaala ya elimu ili kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi wa shirika hilo Tanzania, Agness Hotay akizungumza jijini hapa leo April 17, 2019 wakati akitoa salamu kwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya shirika hilo amesema malengo yao kuwasaidia watoto wenye uhitaji wanaotoka katika familia ambazo hazina uwezo.

Amesema kuwepo kwa somo la ulinzi kwa mtoto kutamsaidia mwanafunzi kujia ni jinsi gani anaweza kujikinga na matukio ya ukatili wa kijinsia kwake.

“Kwenye mitaala shuleni kukiwa na somo la ulinzi kwa watoto itasaidia kukabiliana na matukio ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakitokea kwenye jamii mara kwa mara kwani watoto hao watajua jinsi ya kujiepusha nayo lakini wakipata elimu hiyo wanaielimisha jamii yao,” amesema Hotay.

Amesema shirika hilo lina wajibu wa kuhakikisha kila mtoto bila kujali jinsia, dini au kabila ana uthibitisho kuwa anapendwa, analindwa na kujulikana akisema wana wajibu wa kumtetea mtoto na kusimamia stahiki za mtoto husika ili afikie ndoto zake.

Amesema katika kipindi cha miaka 20 shirika hilo limewafikia vijana 135,750 na hadi sasa vijana 99,671 bado wapo kwenye huduma na 36,133 wametoka kwenye mpango wa kuhudumiwa na Compassion Tanzania.

“Kupitia makanisa ambayo ni washirika wenza tumeweza kutoa ajira zaidi ya 1,300 katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini,” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa, amewasihi viongozi wa dini kutoa elimu juu ya watoto wenye ulemavu ili jamii iweze kuwapa haki sawa na watu wengine.

“Naomba niwasisitize viongozi wa dini kutoa elimu ya uelewa kwa jamii juu ya watu wenye ulemavu ili iwachukulie kama watu wengine na si kuwatenga, ifike hatua hata kwenye mahusiano mtu mwenye ulemavu asikose kuoa au kuolewa kwa kigezo cha kuwa na ulemavu,” amesema Ikupa.

Share.

About Author

Leave A Reply