Sunday, August 25

Sevilla yaja na muuaji wa Manchester United kuivaa Simba

0


By Majuto Omary

Dar es Salaam. Mshambuaji nyota wa Sevilla, Wissam Ben Yedder ni miongoni mwa wachezaji 18 waliowasili leo kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Simba uliopangwa kufanyika Alhamisi kesho kwenye Uwanja wa Taifa.
Mashabiki wa Manchester United ya England wanamkumbuka Yedder ambaye alibadili matokeo ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya mwaka jana, baada ya kufunga mabao mawili mjini Manchester na kuiondosha timu hiyo katika mashindano hayo.
Man United ilichapwa mabao 2-1 kwenye Old Trafford. Mechi ya awali Hispania timu hizo zilitoka suluhu.
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema kuwa mbali ya nyota huyo ambaye amefunga mabao 19 kwenye Ligi ya Hispania iliyomalizika hivi karibuni, pia kuna wachezaji nyota waliocheza na timu kama Real Madrid na Barcelona.
Nyota hao ni  Jesus Navas,  Aleix Vidal, Nolito (Manuel Agudo Durán), Quincy Promes, Franco Vazquez, Sergi Gomez na mlinda mlango, Tomas Vaclik.
Nyota hao wamekuwa nguzo ya timu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi sita kwa kukusanya pointi 59 na kupata nafasi ya kucheza ligi ya Europa League.
Wachezaji wengine ni  Juan Soriano, Simon  Kjaer, Joris Gnagnon,  Sergio Escudero, Guilherme Arana,  Ibrahim Amadou, Roque Mesa, Ever Banega, Bryan Gil, na  Munir El Haddadi.
Wachezaji wengine, Wober, Rog, Carriço, Gonalons na André Silva wameshinda kusafiri kutokana na majeruhi huku Pablo Sarabia ambaye ameifungia timu­ yake mabao 12 kwenye La Liga bado hajapona vizuri majeraha yake.
Tarimba alisema kuwa mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kwani hata Simba imedhamiria kuwachezesha wachezaji wake nyota ambao waliiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya makundi na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Siyo mechi rahisi hata kidogo. Kila timu imedhamiria kuwachezesha wachezaji wake nyota ambao wameshiriki katika Ligi Kuu za nchi hizo mbili. SportPesa Tanzania inajivunia kufanikisha ziara hii ambapo kwa sasa inakuwa kampuni pekee ya michezo ya kubahatisha kuleta timu mbili kutoka bara la Ulaya na kucheza Tanzania,” alisema Tarimba.
Alisema kuwa SportPesa Tanzania imeamua kujikita katika maendeleo ya soka nchini na ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele katika shughuli mbalimbali za kuiunga mkono serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali.
“Tulianza na kuchagia timu ya Taifa ya soka ya chini ya umri wa miaka 17 iliyoshiriki fainali za  Afcon  nchini gabon mwaka 2017 na baadaye kufanikisha zaiara ya timu ya Everton  na baadaye kuufanyia ukarabati uwanja wa Taifa na kutumia Sh1.4 bilioni. Tunajisikia fahari sana kufanikisha ujio wa Sevilla ambao kabla ya hapo, makocha wa timu ya kongwe ya Ligi Kuu ya Uingereza, Southampton waliendesha kozi ya makocha zaidi ya 30 hapa nchini,” alisema Tarimba.


Share.

About Author

Leave A Reply