Wednesday, August 21

Sevilla ya bilioni 700 yaivaa Simba ya bilioni moja

0


By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Wakati Meddie Kagere wa Simba akiwa na thamani ya dola 50,000 (Sh115milioni), mshambuliaji hatari katika kikosi cha Sevilla, Wissam Ben Yedder thamani yake ni paund 31 milioni (Sh90.7 bilioni).

Thamani ya Kikosi cha Sevilla ni paund 257m zaidi ya Sh752 bilioni, ambao watacheza na Simba wenye thamani ya zaidi ya bilioni moja mchezo wa kirafiki Alhamisi.

Sevilla ni miongoni mwa timu bora kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikitesa kwenye soka la Ulaya, ikiwa chini Unai Emery walitwaa mara tatu kombe la Europa Ligi kwenye msimu wa 2013–14, 2014–15, 2015–16.

Vigogo hao, kikosi chao kinamstaa mbalimbali ambao wamefanya vizuri msimu ulimalizika wa Ligi Kuu Hispania ambayo ni maarufu kama La Liga, akiwemo Ben Yedder.

Ben Yedder ambaye ni Mfaransa, ameifungia Sevilla msimu huu mabao 18 na kutengeneza mengine tisa kwenye michezo 35 ya La Liga.

Nyota mwingine tishio kwenye kikosi cha Sevilla ambacho kinanolewa na kocha Joaquín Caparrós ni kiungo, Pablo Sarabia mwenye thamani ya paund 36 milioni (Sh105 bilioni).

Sarabia na Lionel Messi wa Barcelona ndio mastaa ambao msimu huu wa 2018/19, wamepiga pasi nyingi za mwisho zilizozaa mabao ambazo ni 13 kila mmoja.


Share.

About Author

Leave A Reply