Wednesday, May 22

Serikali yaja na mapendekezo mapya faini serikali za mitaa

0


By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imependekeza Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) ifanyiwe marekebisho ili kuongeza adhabu kwa wanaokiuka sheria ndogo ama amri, kutoka faini isiyozidi Sh50,000 hadi isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 ama vyote.

Mapendekezo hayo yako katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2018 uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni juzi.

Muswada huo unalenga kufanyia marekebisho sheria nne. Nyingine ni ya Mafao ya Kustaafu Utumishi wa Siasa, ya Pasipoti na Hati za Kusafiria na Sheria ya Bodi ya Utalii.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi, marekebisho hayo yanalenga kuifanya sheria hiyo kuwa sambamba na masharti yaliyoainishwa kwenye kifungu cha 156(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) sura ya 287.

Katika Sheria ya Mafao ya kustaafu utumishi wa kisiasa, Dk Kilangi alisema marekebisho hayo yanalenga kuondoa masuala yaliyoko katika sheria hiyo yanayohusu haki za viongozi wastaafu kupewa pasipoti.

Alisema marekebisho hayo yanazungumzia masuala yote yanayohusu pasipoti kuwa yatafafanuliwa chini ya Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria na Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika utumishi wa kisiasa sura 225, itabaki na masharti ya mafao ya viongozi.

Share.

About Author

Leave A Reply