Friday, August 23

Serikali yaipongeza SportPesa ujio wa Sevilla, waahidi kutangaza utalii

0


WAZIRI wa Utalii na Maliasili, Dk Hamisi Kigwangala amesema kuwa ujio wa klabu ya Sevilla ni fursa kubwa ya kuitangaza nchi kupitia vivutio vya mali ya asili.

Kauli hiyo, aliitoa leo baada ya Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa kutangaza kuwaleta Sevilla nchini kwa ajili ya ziara ya kimichezo.

Wakiwa nchini, Sevilla ambao pia ni mabingwa mara moja wa La Liga, watacheza na moja ya timu washirika wa SportPesa kati ya Simba au Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kigwangala alisema kuwa ujio wa Sevilla nchini unatosha kabisa duniani kuijua Tanzania kutokana na ukubwa wa klabu hiyo yenye mashabiki wengi.

Kigwangala alisema, hivi sasa watu wengi duniani watataka kuijua Tanzania na kuanza kuonekana kwenye ramani ya dunia, hivyo ni fursa kwa nchi kutangaza utalii uliojaliwa kupitia wachezaji hao.

Alisema kuwa, serikali imepanga kuitumia fursa hiyo kwa kushirikiana na SportPesa kwa lengo la kutangaza vivutio vya nchi kabla na baada ya mechi hiyo kuchezwa kati ya Simba na Yanga.

“Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Utalii na Mali Asili hii ni fursa yetu tunayotakiwa kuitumia vema kuitangaza nchi kupitia ziara ya Sevilla kuwaleta nchini mabingwa hao mara tano wa michuano ya UEFA Europa ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya msimu mpya wa 2019/2020.

“Kwa kupitia kwa Sevilla wenye wachezaji wakubwa wa kimataifa, kutasaidia kuitangaza nchi watakapokwenda kutembelea vivutio vyetu vya asili tulivyojaaliwa hapa nchini zikiwemo mbuga mbalimbali.

“Wachezaji hao watakapokuwa kwenye hifadhi zetu misitu ya mbugani watapiga picha ambazo watazisamba kwenye mitandao ambapo mashabiki watataka kuhoji ni wapi walipo na kwanini wapo kwenye pori lenye wanyama pori baadaye na wao kuvutiwa na kuja nchini.

“Kwa kufanya hivyo, tutaongeza idadi ya watalii kuja nchini kutembelea na ninajua wataka kwenda Zanzibar kutembelea huko, pia ni fursa nzuri ya kutangaza utalii huko.

 “Kwa kupitia ziara hiyo, tumetoa ofa kwa Sevilla kwa kuwapeleka kwenye moja ya hifadhi zetu bure watakapofika hapa nchini” Alimaliza Waziri Kigwangala.

SportPesa ni kampuni ya kimataifa inayojihusisha na michezo na habari za burudani. Kupitia majukwaa yetu tunatoa matokeo ya mechi papo hapo na kwa nchi nyingine tunatoa huduma ya michezo ya kubashiri na ushindi kwa wateja wetu.

Share.

About Author

Leave A Reply