Tuesday, August 20

Serikali yafikiria kupunguza bei ya umeme

0


By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri na Nishati, Dk Medadi Kalemani amesema Serikali inakusudia kufanya mapitio ya bei ya umeme ili ipungue kwa kuwa miradi mingi ya umeme inayofanyika sasa itakuwa inazalisha umeme kwa bei rahisi tofauti na awali.

Dk Kalemani amesema hayo leo Aprili 28, 2019 wakati wa ziara yake kutembelea miradi mbalimbali ya umeme inayoendelea jijini hapa.

Amesema mapitio hayo yatafanyika mara baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya umeme ya Stiglers Gorge, Kinyerezi 3 na miradi ya umeme wa sola na upepo.

“Baada ya kukamilika kwa mradi wa Kinyerezi kwa awamu zote nne, umeme utakaozalishwa ni megawati 1667, Stiglers gorge megawati 2100 na kuna umeme wa upepo na jua megawati 300 hivyo umeme utakuwa wa kutosha,” amesema.

Amesema Serikali inataka kuondokana na uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta mazito na badala yake kutumia nishati endelevu kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama gesi, maji, makaa ya mawe na joto ardhi.

“Wastani wa gharama za umeme kwa kutumia nishati endelevu ni dola 0.11 (Sh252) kwa uniti moja huku kwa kutumia mafuta mazito ikiwa ni Sh546, hivyo baada ya kukamilika kwa miradi hii bei itapungua,” amesema.

Aidha Dk Kalemani ameagiza kuunganishwa kwa megawati 80 ambazo mpaka sasa zimepatikana katika mradi wa upanuzi wa mradi wa Kinyerezi 2 kuliko kusubiri mpaka zitakapokamilika zote 185.

“Hapa nimeambiwa kuwa mpaka sasa mradi ulipofikia unaweza kuzalisha megawati 80 niagize hizo ziunganishwe kwenye gridi moja kabla ya Juni mwaka huu kuliko kusubiri mradi huo utakapokamilika Agosti, hizo megawati 80 zitasadia kuongeza upatikanaji wa umeme kwa sasa,” amesema.

Aidha meneja miradi wa Tenesco, Stephen Manda amesema mradi huo wa upanuzi wa Kinyerezi umefikia asilimia 82 na kukamilika kwake kutafanikisha kituo hicho kufikia uzalishaji wa megawati 335 kwani awali uzalishaji ulikuwa megawati 150.

Imeelezwa kuwa miradi yote itakuwa imekamilika ifikapo 2022 na mradi wa umeme wa sola na upepo utakamilika Agosti, mwakani.

Share.

About Author

Leave A Reply