Wednesday, August 21

Serikali kutowadai kodi ya majengo wazee

0


By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Manyara, imesema wazee wasiojiweza wenye umri wa kuanzisha miaka 60 na kuendelea hawapaswi kulipa kodi ya majengo.

Ofisa wa elimu ya mlipa kodi wa TRA mkoani Manyara, Nicodemus Masawe ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya mlipa kodi yaliyofanyika leo Jumamosi Mei 18, 2019 mjini Babati.

Masawe amesema wazee wasiojiweza wenye umri huo na kuendelea hawapaswi kulipa kodi ya majengo kwani Serikali imewasamehe.

“Ila wale wazee ambao wanaingiza kipato kupitia nyumba za biashara wanapaswa kulipa kodi, kwani kuna mzee ana miaka zaidi ya 60 lakini ana nyumba tatu au nne za biashara huyo lazima alipe kodi ya majengo,” amesema Masawe.

Naye Kaimu Meneja wa TRA mkoani Manyara, Pius Bugenyi, amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya nchi.

“Kodi ya mapato ndio inasababisha uwapo wa miradi ya sekta mbalimbali hata kwenye vitabu vya dini imeandikwa ya Mungu apewe Mungu na ya Kaizari apewe Kaizari,” amesema Bugenyi.

Mkazi wa mtaa wa Nyunguu mjini Babati, Fatma Hassan amesema TRA wanapaswa kuendelea kutoa elimu ili jamii izidi kupata uelewa mzuri wa suala hilo.

“Kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao hatuna uelewa wa ulipaji kodi lakini tukiwa tunaelimishwa kwa ufasaha tutashiriki ipasavyo kwa nia moja ya maendeleo,” amesema Fatuma.

Share.

About Author

Leave A Reply