Sunday, August 25

Serengeti si riziki, Cecafa majanga U17

0


By THOMAS NG’ITU

KUSHNEI! Safari ya Serengeti Boys katika Fainali za Afrika (Afcon) U17 imefikia tamati rasmi jana Jumamosi baada ya timu hiyo kufungwa mabao 4-2 na Angola, huku Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ikishindwa kupeleka timu kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Vijana nchini Brazili.

Wakati Serengeti ikiaibishwa kwa kuwa timu kibonde kwenye kundi lao kwa kushindwa kuambulia japo pointi moja, wawakilishi wengine wa Cecafa, Uganda walijikuta wakilazimishwa sare ya 1-1 na vinara wa Kundi A Nigeria na kukwama kufuzu nusu fainali na kwenda Brazili kwenye Fainali za Dunia U17.

Angola na Nigeria ndizo zilizofuzu kupitia Kundi A kucheza hatua inayofuata sambamba na kukata tiketi ya kwenda Brazili, wakiungana na Cameroon kutoka Kundi B iliyotangulia mapema.

Katika mchezo wa jana uliopigwa Uwanja wa Taifa, Serengeti walianza kwa kuwachanganya vijana wa Angola na hii ilitokana na mfumo walioutumia wenyeji wa 4-3-3 kutoka ule waliokuwa wakiutimia wa 4-4-2.

Kocha Oscar Mirambo aliwaanzisha Agiri Ngoda, Kelvin John na Edmund John katika eneo la ushambuliaji kiasi ambacho kiliwafanya kuonekana bora kutokana na Ngoda na Kelvin kutokea pembeni wakilazimisha safu ya ulinzi ifanye makosa.

Dakika 12 tu ya mchezo Serengeti walipata goli kupitia kwa Omary Juma baada ya kutumia uzembe wa mabeki wa Angola, lakini Waangola walirejesha bao hilo dakika ya 17 kupitia Mimo na dakika nne kabla ya mapumziko, Omary alimkata Capemba ndani ya 18 na mwamuzi kuamuru penalti.

Penalti hiyo iliyokwamishwa wavuni na Capemba, lakini dakika mbili tu baadaye Serengeti walisawazisha bao hilo 43 kupitia Ngoda baada ya mabeki wa Angola kujichanganya na yeye kupiga shuti kali lililoenda moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa 2-2.

Kipindi cha pili Angola walikuja kivingine na kupata mabao mawili kupitia kwa David dakika ya 68 kabla ya Capemba kuongeza la nne dakika ya 72 na kuihakikishia timu yake nafasi ya kuungana na Nigeria kucheza nusu fainali zinazoanza Jumatano ijayo.

Katika mchezo uliopigwa Azam Complex, Uganda na Nigeria zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya ba0 1-1, Uganda wakiwa wa kwanza kupata bao dakika ya Alou JK dakika ya 69 kabla ya Nigeria kuchomoa kupitia kwa Jabaar Ibraheem dakika ya 74.

Timu ya mwisho ya kukamilisha idadi ya timu za nusu fainali itajulisha leo wakati mechi za Kundi B zitachezwa, Cameroon kuvaana na Senegal na Guinea kuvaana na Morocco mechi zote zikitarajiwa kucheza saa 10:00 jioni.

Share.

About Author

Leave A Reply