Sunday, August 25

Serengeti Boys mshumaa uliozimika mbele ya halaiki

0


By Oliver Albert

Kuna maeneo matatu tunayoweza kuiangalia timu ya taifa ya vijana ya Tanzania, Serengeti Boys iliyoshiriki Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.

Kati ya timu zilizoshiriki, Serengeti Boys ndiyo iliyofanya vibaya zaidi kuliko timu zote wakati ndiyo mwenyeji wa fainali za mwaka huu.

Kwanza; ndiyo mnyonge wa timu zote, imefungwa mabao 12-6, ikiwa ni 5-4 na Nigeria, 3-0 na Uganda na ikalala 4-2 kwa Angola.

Hakuna kilichokuwa kimekosekana kwenye hamasa. Watanzania wali

hamasika kwelikweli na timu hata kuwepo na kampeni ya kuwaunga mkono kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Walipata sapoti ya maana.

Kimsingi, timu ni kama haikuandaliwa kabisa wala kuwa tayari kwa fainali hizi ikilinganisha na fainali za Afcon 2017 ambazo Tanzania ilitoka suluhu na Mali waliokuwa mabingwa, ikaifunga Angola mabao 2-1 na baadaye kulala 1-0 kwa Guinea.

Ukakamavu wa kikosi ulichangia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri fainali zile za Gabon.

Tanzania ni mwenyeji wake lakini Serengeti Boys ikiwa ndio ‘mwenye nyumba’ imeaga mapema kwa kupoteza michezo yote mitatu kutoka Kundi A.

Timu hiyo mwenyeji iliungana na ndugu yake kutoka Kanda ya Afrika Mashariki, Uganda kuaga fainali hizo na kuziacha Angola na Nigeria zikifuzu nusu fainali kutoka Kundi lao la A.

Sio tu kutolewa mapema lakini Serengeti Boys imekosa nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil kuanzia Oktoba 5 hadi 25, mwaka huu.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha mzawa Oscar Mirambo kimeondoshwa katika fainali hizo na zaidi kuonekana kukosa uzoefu wa Fainali hizo tofauti na timu nyingi ambazo zimekuwa zikishiriki mara kwa mara.

Kocha wa Serengeti Boys amejitetea kuwa uzoefu umewakwamisha kufanya vizuri lakini anaamini wachezaji wake wamepata kitu cha kujifunza.

Hata hivyo, pamoja na kukaa na timu muda mrefu, Serengeti Boys ilishtua Watanzania hasa ilipofungw amabao 5-0 na Uturuki kwenye mechi za Uefa Assist. Haikufanya vizuri katika mashindano yale kwani ilianza kwa kuchapwa bao 1-0 na Guinea na kupata ushindi wa mbinde na Australia wa mabao 3-2.

Kocha Mirambo alilalamikiwa kiwango cha timu yake na kusema wameona tatizo na watalifanyia kazi. Watanzania walianza kufuatilia kwa umakini timu ilipokuwa Uturuki wakaona tatizo ni kipa na ngome kuvuja.

Serengeti Boys vs Nigeria

Ulikuwa mchezo wa kwanza wa kufungua pazia la Fainali za Afrika kwa vijana (Afcon) na ambao ulizalisha mabao mengi kuliko mchezo mwingine wowote katika fainali hizo.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi Serengeti Boys ililala kwa mabao 5-4.

Katika mchezo huo Serengeti Boys licha ya kuonyesha kiwango safu ya ushambuliaji lakini safu ya ulinzi ilikuwa na tobo huku kipa Mwinyi Yahya ikikosa umakini langoni na kufungwa mabao mepesi.

Mabeki wa Serengeti Boys walionekana kuzembea katika ukabaji na kuwaruhusu Nigeria kuuchezea mpira. Waliocheza soka la kasi hata kufika golini kwa Serengeti wanavyotaka.

Bao la kwanza la Nigeria lilitokana na uzembe wa mabeki licha ya kipa Mwinyi Yahya kupangua shuti lililopigwa na Wisdom Ubani kabla ya Olatomi Olaniyani kufunga kirahisi.

Pia bao la pili nalo lilitokana na uzembe wa mabeki ambao walikuwa wakizidiwa kasi na Wanigeria hivyo kumuacha mfungaji wa bao hilo Wisdom Ubani akiwa peke yake na kufunga.

Nigeria walifunga bao la tatu kupitia kwa Akinkunimi Amoo ambaye mabeki wa Serengeti Boys walishindwa kumzuia na ambao walipigwa chenga na mfungaji huyo huku bao la nne likifungwa kwa faulo ya moja kwa moja na bao la tano likifungwa nje kidogo ya 18.

Mirambo alisema malengo yao yalikuwa kushinda lakini bahati mbaya matokeo yakaja tofauti.

“Lazima watu wajue kwamba tunahusika na watoto wadogo hivyo kama unawaongoza watoto huwezi kutegemea kupata ufanisi kwa kiwango kile unachotaka muda wote.

“Washambuliaji wamefanya kile ambacho wameweza kufanya na timu imefanya kile ambacho kinawezekana. Makosa kwenye mpira wa miguu yapo na kazi tuliyo nayo ni kuangalia wapi na eneo gani kuna maendeleo mazuri na sehemu gani kuna shida.

“ Ukiangalia vitu vililvyotokea katika mechi hiyo ni vile tulivyokuwa tulikuwa tunavifanyia kazi kila mara lakini tulifanya sana makosa.

“Tunapopoteza mpira tunakuwa tunaridhika na hivyo kutafuta mpira tunachelewa hivyo kujikuta sehemu kubwa tunafanya kazi ya kukaba.

“Kipa anaweza kuwa na makosa lakini hatuwezi kumuacha kwa sababu tunapompa tena nafasi kipa ambaye alikuwa akifanya makosa tunatarajia kuwa anaimarika.

“Licha ya kwamba hawa watoto wanafanya makosa hatuwezi kukata tamaa zaidi ya kuwaelekeza kila mara ingawa mwisho wa siku inatugharimu,” anasema Mirambo.

“Pengine kuna somo la kujifunza kwenye hilo kuliko kuona tumekosea kitu gani. Kwenye kipa kuna changamoto na kila mmoja ameona lakini kama tutaweza kufanya vizuri kuanzia katikati ya uwanjani mpaka kwenye mabeki basi matatizo ya kipa yatakuwa madogo

“Hiyo nafasi ina changamoto kwa sababu kile ambacho kinashindikana kwenye kiungo na mabeki unategemea kisahihishwe na kipa kwani huwezi kucheza dakika 90 mpira usifike golini kwako .

Katika mchezo huu kocha Mirambo alibadilisha kipa na kumwanzisha, Shaaban Hassan badala ya Mwinyi Yahya huku pia akiwapumzisha viungo Mustafa Nakuku na Misungwi Chananja na kuwachezesha Edson Mshirakandi na Ladaki Chasambi.

Hata hivyo, katika mcheoz ambao safu ya kiungo ilicheza ovyo basi ni katika mchezo huu kwani Serengeti Boys ilishindwa kutengeneza nafasi za mabao na kujikuta ikiambulia kichapo cha mabao 3-0.

Mabeki waliendelea kuiangusha Serengeti boys hata katika mchezo huo baada ya kumuacha Andrew Kawooya akifunga bao jepesi huku mabeki wakimtazama tu.

Bao la pili lililofungwa na Ivan Asaba nalo lilichangiwa na uzembe wa mabeki kushindwa kumkaba Najib Yaga ambaye alitoka na mpira nje ya 18 na kupenyeza pasi kwa mfungaji. Bao la tatu lilifungwa na Yaga kwa kichwa huku akionekana kuruka peke yake bila hata mabeki kumbugudhi.

Baada ya mchezo huo kocha Mirambo alisema: “Hatukutengeneza nafasi nyingi kama tunavyokuwa kila wakati na ndio maana hatukupata bao.

“Bado kuna kazi ya kufanya hatuwezi kukata tamaa. Kila mara tunaimarika na mwisho wa siku tunaamini tunatengenea wachezaji ambao baadaye watakuwa na faida kwa Taifa.

Tatizo lilelile la udhaifu wa safu ya ulinzi lilieendelea kuitesa Serengeti Boys katika mechi hii na kujikuta ikipokea kipigo cha mabao 4-2.

Kosa la kwanza la safu ya ulinzi ya Serengeti Boys katika mchezo huo lilifanyika dakika ya 17 baada kumruhusu mchezaji Telson Tome kuruka akiwa mwenyewe na kuunganisha mpira wa kona ambao uliipatia Angola bao la kusawazisha.

Bao hilo la kusawazisha la Angola lilikuja ndani ya dakika tano tu baada ya Serengeti Boys kupata bao la utangulizi kupitia kwa Omary Omary aliyefunga dakika ya 12

Kiungo Arafat Swakali dakika ya 41 alifanya makosa ya kizembe kwa kupoteza mpira kwa viungo wa Angola na kisha kucheza faulo ndani ya eneo la hatari ambayo ilisababisha penalti iliyofungwa na Osvaldo Capemba

Hata hivyo, dakika moja kabla ya mapumziko, Agiri Ngoda aliisawazishia Serengeti Boys baada ya kuunganisha vyema pasi ya Kelvin John.

Kipindi cha pili, mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi kwani uzembe wa mabeki kushindwa kumdhibiti winga msumbufu wa Angola, Zito Luvumbo ulizaa bao la tatu kwa Angola dakika ya 68 baada ya winga huyo kupiga krosi nzuri iliyomaliziwa vyema na David Mzanza.

Tatizo la mabeki na kipa.

1. Swali lililopo, benchi la ufundi lilikuwa linajiandaa na nini kama timu yenyewe ilikuwa na matatizo ya kipa na mabeki?

2. Je kocha Mirambo alifanya jitihada gani kupata kikosi mbadala baada ya wachezaji wake tegemeo kukumbwa na MRI?

3. Ilikuwaje Mirambo aliendelea kukaa na wachezaji wanaoondoka kwenye sifa za kuzaliwa wakati walishaelezwa wanatakiwa waliozaliwa mwezi na mwaka fulani?

Alipoulizwa je kutokana na matokeo hayo kwa nini asijiuzulu, Mirambo alijibu: “Hata mimi, nimehuzunishwa, sio Watanzania tu kwani sikutaka kupata matokeo haya ambayo nimepata.

“Hakuna mtu anayefurahi kwa haya matokeo na kung’atuka au kutokung’atuka sio tatizo kwani hata kama niking’atuka leo itabadilisha nini.

“Kukimbia matatizo sio kutatua matatizo na pia mimi sio ninayefanya uamuzi kama natakiwa kuwepo au kuondoka kwenye timu kwa sababu sikujipa mwenyewe nafasi ya kubakia kwenye timu.”

Share.

About Author

Leave A Reply