Wednesday, June 19

Scholes amchefua kocha Mourinho

0


Manchester, England. Kocha Jose Mourinho, amesema pamoja na kukoselewa na watu wengi hajapata kuumizwa na wakosoaji hao tangu ameanza kuinoa Manchester United kama alivyoumizwa na Paul Scholes.

Mourinho raia wa Ureno, ambaye bado hajapata matokeo yaliyotarajiwa ndani ya Man United katika miaka yote mitatu ya kazi hapo Old Trafford.

Scholes aliyeitumikia Man United michezo 717, amekuwa mmoja wa wakosoaji wa Mourinho, akisema ni kocha aliyeshindwa kuudhibiti mdomo wake mchafu.

Kiungo huyo wa zamani wa Man United na anayependwa na kuheshimiwa na mashabiki wa klabu hiyo, alisema domo chafu la Mourinho ndilo linaloikosesha timu ufanisi.

Alimponda kocha huyo akisema, anaenda kinyume na utamaduni wa klabu kwani amekuwa akitibuana na wachezaji kila siku, jambo linalowapunguzia morari wa kusaka ushindi dimbani.

Scholes alisema anaamini hilo ndilo lililomfanya asipate mafanikio Chelsea aliporudi kwa mara ya pili na pia Real Madrid ambako alishindwa kumaliza mkataba wake.

“Nadhani Mourinho ni mtu asiyejiheshimu asiyeuchunga mdomo wake, ndiye anayesababisha timu isipate matokeo mazuri,” alisema Scholes.

Kocha huyo pia alielezea kukerwa na tabia iliyozushwa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kumzomea yeye na kikosi chake wawapo dimbani.

Timu hiyo leo ipo ugenini ambako itakipiga na Juventus katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, katika mechi ya kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Old Trafford, Man United ilifungwa bao 1-0.

Man United ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne tano nyuma ya vinara Juventus, ambayo inahitaji sare tu kama sio ushindi leo ili kujikatia tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora.

Share.

About Author

Leave A Reply