Friday, July 19

Samia azitetea taasisi za Serikali zinazodaiwa zisikatiwe maji

0


Babati. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Babati (Bawasa) mkoani Manyara kutozikatia maji taasisi za Serikali zinazodaiwa ila washirikiane na mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na kufikisha madai yao Hazina ya Sh206.8 milioni.

Makamu wa Rais  ameyasema hayo leo mjini Babati wakati akizindua jengo la Bawasa lililogharimu Sh2.48 bilioni lililoanza kujengwa mwaka 2010 na kukamilika mwaka 2016.

Amesema kuliko kuzikatia maji taasisi za Serikali ikiwamo magereza, polisi na hospitali ni bora kushirikiana na mkuu wa mkoa na kuandika madai yao Hazina ili zilipwe kupitia fedha za matumizi wanazopatiwa.

“Siyo jambo zuri kuwakatia maji ila mkiandika Hazina watakuwa wanawalipa fedha hizo kwani zitakuwa zinakatwa moja kwa moja kwao, jaribuni kufanya hayo mtaona manufaa yake,” amesema.

Awali, mkurugenzi mtendaji wa Bawasa, Iddy Msuya alisema baadhi ya taasisi za Serikali magereza na polisi zinadaiwa ankara za maji kwa zaidi ya miaka miwili Sh206.8 milioni.

Aidha, alisema baadhi ya wananchi wanakataa kuachia maeneo ya vyanzo vya maji na kuendelea kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.

Alisema wanatoa shukrani na kuipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuhakikisha huduma ya maji inafikia asilimia 95 mwaka 2020 kwa kutenga Sh2 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Alisema idadi ya wakazi wa mji wa Babati wanaopata maji imeongezeka kutoka asilimia 53 Desemba mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 75 Novemba 2018 na kwamba pia kuna ongezeko la idadi ya wateja waliounganishwa huduma ya maji mjini Babati kutoka 5,550 Desemba mwaka 2015 hadi kufikia 8,060 Novemba 2018.

Mnyeti alisema wapo tayari kufuatilia maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais ili kuhakikisha yote yanatekelezwa.

Alisema Bawasa kwa kiasi kikubwa inatekeleza wajibu wake ipasavyo katika kuhakikisha wananchi wa mji wa Babati wanapata maji pamoja na miji midogo ya Mbulu, Katesh, Orkesumet na Mirerani.

Share.

About Author

Leave A Reply