Friday, August 23

Ripoti ya CAG yaibua madudu taasisi za Serikali

0


Dar es Salaam. Ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ya mwaka 2016/17 imeibua ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika taasisi za Serikali.

Pamoja na kubainisha kasoro hizo, ripoti hiyo imeonyesha kuimarika kwa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kwani, ikisema mashirika ya umma yamepata hati safi kwa asilimia 96, Serikali za Mitaa asilimia 90 ambako ni halmashauri tatu tu zilizopata hati chafu na Serikali Kuu ikipata hati safi kwa asilimia 86.

Baada ya kuipokea, Rais John Magufuli aliahidi kuifanyia kazi mara moja na kuwachukulia hatua viongozi watakaobainika kuhusika.

Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam jana, imezitaja taasisi zilizobainika kuwa na ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha kuwa ni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Nyingine ni iliyokuwa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambacho kilichunguzwa licha ya kutokuwa shirika la umma.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Profesa Assad alisema, “Mfano TRA kuna upungufu unaotokana na kesi za muda mrefu za kodi zilizopo mahakamani zinazofikia Sh4.4 triolini na upungufu katika kushughulikia mapingamizi ya kodi yaliyofikia Sh739 bilioni.

“Mifumo ambayo hairidhishi katika udhibiti wa mizigo inayopita nchini kwenda nchi nyingine, lita milioni 26 za mafuta ambayo kodi yake ilifikia Sh14 bilioni ambazo hata hivyo, hazikusafirishwa kwenda nje ya nchi na zilitumika nchini,” alisema.

Alisema mitambo ya uchenjuaji wa madini katika mikoa ya Mwanza na eneo la Kahama, Shinyanga inayofikia 84 inafanya kazi bila leseni na kusababisha ukosefu wa maduhuli katika Serikali ya Sh232 milioni.

Kuhusu Rahco alisema, “Imefanya upembuzi yakinifu uliogharimu Sh20 bilioni, kwa sababu ya kukosa fedha, imeishia kufanya upembuzi yakinifu, sasa ukifanya upembuzi bila kufanya mradi wenyewe unakuwa umepoteza fedha.

“TRA walishindwa kuwasilisha mapato ya reli yanayofikia Sh194 bilioni yaliyotakiwa kwenda Rahco na hayakwenda mpaka leo,” alisema.

Kwa upande wa MSD, Profesa Assad alisema kulikuwa na dawa zilizoisha muda wake zinazofikia Sh4.5 bilioni ambazo alisema ukaguzi wake ulibaini kuwa ni tatizo.

Akizungumzia NSSF, alisema iliingia mkataba wa kutoa mkopo na taasisi nyingine nne wa Sh60 bilioni, lakini ililipa Sh67 bilioni, ikiwa ni zaidi kwa Sh7 bilioni bila kuwa na mkataba na huenda kiasi hicho cha fedha kikapotea.

Kwa TPA alisema, “Usimamizi wa kitengo cha makontena bandarini Ticts hautoshelezi, si madhubuti kwa sababu TPA wanashindwa kupata kipato kinachostahili kwa kila kontena linaloingia pale hivyo lazima kuboreshwa.”

Profesa Assad alisema waliombwa kufanya ukaguzi maalumu CWT na kubainisha kuwa, “Sehemu kubwa tuliona hii taasisi haiendeshwi sawasawa kulikuwa na mambo yanafanyika kinyume cha kanuni za fedha.

“Mfano, malipo ya Sh3.5 bilioni yaliyofanyika bila kuidhinishwa na katibu mkuu au mweka hazina wa CWT kati ya mwaka 2011 na 2016. Usimamizi usiofaa katika Benki ya Walimu na Mwalimu House, huwezi kuona umiliki wa moja kwa moja.”

CAG alisema Nida kwa upande wake, kulikuwa na ubadhirifu kwenye ukodishaji wa eneo la ofisi lililoonekana kuwa na mita za mraba 2,200, lakini lilipopimwa walibaini kuwa ni mita 1,945. Hivyo kuwapo mita hewa za mraba 254 zenye thamani ya Sh402 milioni kwa sababu ya uzembe.

Alisema Nida ilipata hasara ya Sh167 milioni kwa kutegemea viwango vya benki za biashara badala ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Huwezi kutegemea riba ya benki ya bishara badala ya Benki Kuu,” alisema.

Kwa UDSM alisema malipo ya dola161,332 za Marekani (zaidi ya Sh362 milioni) yalifanyika bila mkataba rasmi.

Kuhusu miradi ya maendeleo, Profesa Assad alisema fedha za ushuru wa mafuta na usafirishaji zilizokusanywa na TRA zinazofikia Sh15 bilioni zilizopaswa kufikishwa katika Mfuko wa Barabara hazikufika.

Alisema Mfuko wa Barabara haukulipa fidia ya Sh12 bilioni kwa walioathirika na miradi ya barabara pamoja na malipo ya riba ya makandarasi yanayofikia Sh4 bilioni zilizocheleweshwa kutoka Hazina.

CAG alizungumzia pia malipo ya matibabu nje ya nchi hasa India akisema yamefikia Sh46 bilioni, “Hizi fedha ni nyingi sana kama hakuna mpango wa kulipa kidogokidogo, mwisho tunaweza kunyimwa huduma.”

Kuhusu ununuzi, alisema kuna udhaifu katika usimamizi wa mikataba ndani ya Serikali Kuu. Alitoa mfano akisema taasisi saba zilifanya ununuzi wa Sh3 bilioni bila kuidhinishwa na bodi.

Alisema taasisi 11 zilinunua bidhaa za huduma za ujenzi za Sh1.5 bilioni kutoka kwa wazabuni bila kuwa na mikataba.

Alisema taasisi 14 zilinunua na kupokea bidhaa na huduma zenye za Sh1.7 bilioni bila kukaguliwa na kamati husika kinyume na kanuni ya ununuzi wa umma ya mwaka 2013.

Ahadi ya JPM

Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti hizo, alimkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kumuagiza akae na mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa taasisi mbalimbali akiwamo CAG ili kupitia hoja zilizomo.

“Ripoti tumezipokea na tutazifanyia kazi kwelikweli kwani yako baadhi ya mambo mengine yanasababishwa na watendaji wetu. Tusipoanza kuchukua hatua hatuwezi kufika, basi tunaanza kuchukua hatua, haiwezekani hizi halmashauri zikatutia aibu nchi nzima.

“Tunaomba hizi kesi za kodi, Jaji Mkuu (Profesa Ibrahim Juma) yupo, Waziri wa Fedha (Dk Philip Mpango) yupo, kaeni mzione hizi, sijajua taratibu zenu za mahakama, najua kuna upungufu wa majaji, lakini katika hili naomba unisaidie ili tuokoe hizi Sh4.4 trilioni.”

Aliwaahidi pia wenyeviti wa kamati za Bunge kuwa ushauri wao utafanyiwa kazi na kuwaambia, “Kuna hoja nyingine huwa za miaka 20, tutengeneze utaratibu ili zisiwe zinajirudiarudia na kama wapo watu sugu, mwaka huu waliambiwa, wataambiwa tena, leteni mapendekezo ili tumtoe akapumzike.”

Wenyeviti wa kamati za Bunge

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Dk Raphael Chegeni alimuomba Rais Magufuli kujaza nafasi ambazo zinakaimiwa, zikiwamo za bodi za taasisi na mamlaka pamoja na ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Tunatoa mapendekezo mengi kamati ya PAC yakitokana na mapendekezo ya CAG lakini hakuna chombo kinachofuatilia utekelezaji wake na kuna uzembe unaojirudia mara kwa mara,” alisema Naghenjwa Kaboyoka, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Vedasto Ngombale alisema kwamba kati ya halmashauri zaidi ya 180, wamefanikiwa kuhoji zisizozidi 40 na kuomba kuongezewa uwezo ili wakague zaidi kubaini ubadhirifu wa fedha za Serikali.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.