Tuesday, August 20

RC Tanga aja juu mimba, unyanyasaji wanafunzi

0


By Rajabu Athumani,Mwananchi [email protected]

Handeni. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela ameonyesha kukerwa na kitendo cha baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji,  mitaa, kata mpaka tarafa kwa kushindwa kutatua kesi za wanafunzi kunyanyaswa kijinsia na mimba za wanafunzi katika maeneo yao.

Akizungumza wakati akipokea maoni ya viongozi mbalimbali kwenye kikao cha maadhimisho ya juma la elimu kimkoa lililofanyika wilayani Handeni Aprili 27, mkuu huyo wa mkoa alisema anasikitishwa kuona mwananchi (mwanafunzi/mzazi) anatoka mbali mpaka kufika kwa mkuu wa wilaya lakini alikotoka kuna viongozi.

Amesema taarifa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah kuhusu mwanafunzi wa umri wa miaka 14 kunyanyaswa kijinsia lakini hakupata msaada katika eneo lake mpaka kufika ofisi ya mkuu huyo wa wilaya, eneo husika kuna tatizo.

“Najaribu kuwaza. Mwanafunzi wa miaka 14 ananyanyaswa kijinsia na kupata mimba lakini viongozi wa eneo husika hawana taarifa yoyote, hili haliingii akilini lazima kuna tatizo kwa viongozi husika, “amesema Shigela.

Kutokana na hilo, mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi wote wa ngazi za vijiji, mitaa, kata na tarafa kufuatilia kwa karibu matukio yanayowakuta wanafunzi katika maeneo yao.

Katika kikao hicho mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainab alisema amesikitishwa kwa kitendo alichofanyiwa mmoja wa wanafunzi kwenye wilaya yake huku viongozi wenzie wakiwa hawafahamu lolote mpaka kesi hiyo kufika kwake.

Ameshauri kamati zote zinazohusika na kufuatilia masuala ya wanafunzi kushirikiana na kupeana taarifa ili kuhakikisha kila mmoja anapata taarifa na kuifanyia kazi hasa masuala ya wanafunzi.

Viongozi mbalimbali wa wilaya za mkoa wa Tanga wamekutana wilayani Handeni katika maadhimisho ya juma la elimu kimkoa ambalo linafanyika wilayani humo.

Share.

About Author

Leave A Reply