Tuesday, August 20

RC Gambo asema Lema na meya sasa wamekubali kazi ya JPM

0


By Mussa Juma,Mwananchi [email protected]

Arusha. Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, wamebadilika na sasa wamekuikubali kazi nzuri inayofanywa na Rais John Magufuli.

Akiwakaribisha Lema na Calist kusalimia katika hafla ya uzinduzi wa maabara ya kisasa ya Tume ya Nguvu za Atomic jijini hapa leo Jumatatu Aprili 29, 2019, Gambo amesema hivi sasa Lema na Lazaro ni marafiki zake.

Amesema viongozi hao wa kisiasa wametambua kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na Serikali na wameamua kuiunga mkono.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, mbunge Lema ni rafiki yangu… ni miongoni mwa watu wachache ambao walikuwa hawaamini kama Rais wetu ana dhamira njema kuibadilisha nchi lakini sasa amekubali na nampongeza kwa kusoma vizuri alama za nyakati,” amesema.

Akimkaribisha Lazaro, Gambo pia alisema ni rafiki yake na akamtaka kumuunga mkono Lema kuendelea kuuunga mkono jitihada za Serikali.

Hata hivyo, Lema akizungumza katika hafla hiyo, ameeleza kuwa alipopata mwaliko wa kuhudhuria hakujua kama kuna jambo kubwa limefanyika lakini baada ya kutembelea maabara na kupata maelezo amejifunza vitu.

Lema amesema kwa sasa yupo likizo ndefu hivyo atakuwa Arusha na akamuomba Waziri Mkuu kama atakuwa na muda aendee kuwa naye Arusha.

Akizungumzia urafiki wa Gambo, amesema leo ni mara ya tano mkuu wa mkoa kusema yeye ni swahiba wake na basi waendelee hivyo hivyo lakini asiwatumie kamati ya ulinzi na usalama kumnyaminya.

“Nilipomwambia hili alikubali na nadhani leo anaweza kukubali mbele yako,” amesema.

Naye Lazaro alisema Gambo ni rafiki yake lakini  alichozungumza leo si wakati wake na akapongeza kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Nguvu za Atomic kujenga maabara hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige, alieleza kuwa Lema asiwe na hofu na likizo kwani yeye ataendelea kuwawakilisha vyema wakazi wa Arusha na kero zao zitapatiwa ufumbuzi.

Jimbo la Arusha ni miongoni mwa majimbo ambayo ni ngome ya upinzani hadi sasa halmashauri ya jiji inaongozwa na Chadema.

Share.

About Author

Leave A Reply