Friday, August 23

Rais Magufuli alivyoshika zamu kukusanya sadaka Mbeya

0


By Godfrey Kahango na Herieth Makwetta, Mwananchi

Mbeya/Dar. Rais John Magufuli jana alinogesha misa takatifu ya kumsimika Gervas Nyaisonga kuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya baada ya kuchukua beseni na kuanza kukusanya sadaka kwa waumini.

Muda wa kutoa sadaka ulipofika, ulitolewa utaratibu wa namna ya kushiriki tendo hilo na wahudumu walichukua mabeseni na kuanza kuzunguka kuwafuata waumini kwa ajili ya kutoa sadaka zao badala ya wao kuinuka mahali walipo kwenda kutoa sadaka hizo.

Moja ya beseni liliwekwa mbele ya jukwaa la wageni rasmi na baada ya Rais Magufuli kuliona, aliinuka kwenye kiti chake akalisogelea na kutoa sadaka yake na kisha akalichukua beseni hilo na kuanza kulipitisha kwa viongozi waliokuwa kwenye jukwaa lake.

Baada ya kumaliza kwa viongozi hao, Rais Magufuli alianza kuzunguka kwa waumini wengine jambo ambalo liliamsha shangwe na vigelele na huku waumini wakigombania kutaka kumsogelea ili kutoa sadaka zao.

Mmoja wa waumini hao, Joseph Emmanuel alisema kitendo cha Rais Magufuli kuungana na wahudumu wengine kuwafuata waumini kukusanya sadaka kimewafurahisha na kunogesa sherehe hiyo kwani waliona ni jambo la shangwe.

“Kwenye mikusanyiko mikubwa kama hii ni utaratibu wa kawaida kabisa watu wahudumu kuchukua beseni na kuwafuata waumini walipo. Lakini kitendo cha Rais wetu kuamua kuchukua beseni na kuwafuata waumini wengi tumefurahi sana,” alisema.

Akizungumza katika misa hiyo, Rais Magufuli alisema alipokuwa mdogo alitamani kuwa askofu au padri.

“Hata waimbaji walipokuwa wakiimba wamenikumbusha wakati nilipokuwa na ndoto hizo, nikawa najiuliza nilikosea wapi, yangekuwa masharti yanalegezwa, ningemuomba Baba Askofu Nyaisonga nikawe padri ili niweze kulihubiri na kulitangaza neno la Mungu ambalo ni la muhimu katika maisha yetu hapa duniani.

“Mapadri ninawaonea wivu, nilitamani niwe huko, kwa hiyo ninyi ambao mpo huko msitoke mpo pazuri. Mimi nilitamani niwe huko lakini nipo huku leo natamani nije huko, nimejisikia raha sana hiyo sadaka niliyokusanya mkaihesabu vizuri,” alisema.

Alisema uaskofu ni daraja takatifu na wito kutoka kwa Mungu, hivyo ni kazi ngumu yenye changamoto zake.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba.

Aliahidi kuwa itaendelea kushirikiana na dini na madhehebu yote kwa sababu ni taasisi nyeti na muhimu kwa jamii kwa sababu zinasaidia kuwafanya wananchi kuwa raia wema.

“Licha ya tofauti zetu za kidini, sisi ni wamoja na hii ndiyo moja ya hazina tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili na taasisi za dini ni wadau wakubwa wa maendeleo,” alisema Rais Magufuli.

Awali katika mahubiri, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo aliwataka waumini kutafakari nini maana ya cheo walichokipata ndani ya kanisa na majukumu yao.

Alisema linahitajika kanisa linaloshirikiana na Serikali katika kuweka mazingira yanayotakiwa.

Alisema Kanisa pekee haliwezi kuwaweka pamoja vijana na kuwapa nidhamu ya kutokulewa kabla ya saa tatu asubuhi lakini Serikali inaweza kufanya hivyo.

“Kwa sababu kazi iliyo njema na inayowapa vijana wetu nidhamu ya kutokulewa kabla ya saa tatu asubuhi ni ile inayowezekana tu kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, neno hilo ni la muhimu kila mtu kulitambua,” alisema Kadinali Pengo.

Akitoa salamu za shukrani baada ya kusimikwa, Askofu Mkuu, Nyaisonga alisema; “Moyo wangu umejaa shukrani kwenu nyote sababu haya matendo makuu niliyojaliwa na Mungu yamechangiwa na mchango wenu kwani mmeshiriki kimwili, kiroho na kwa zawadi mlizotoa.

“Ahadi yenu ya kuniombea itanitengeneza katika utume huu niliokabidhiwa hivi leo, nathamini mchango wenu nyote. Namuomba Mungu atuunganishe tushirikiane ili kwa matendo kwa maneno yetu kwa mawazo yetu watu wote wawe na uzima tele.”

Share.

About Author

Leave A Reply