Wednesday, August 21

Rais Kenyatta aja na mkakati mpya wa uchumi wa kidigitali

0


Kigali. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewafunda viongozi wenzake kuhusu umuhimu wa uchumi wa kidigitali katika maendeleo ya wananchi.

Kiongozi huyo alisema hayo kwenye mkutano wa pili wa kuibadilisha Afrika unaofanyika Kigali nchini Rwanda kwamba bila kutumia digitali mapinduzi ya uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja hayatafika haraka.

Nguzo tano za angalizo la mpango huu wa kidigitali ni kubadilisha huduma zinazotolewa na serikali zifanyike kidigitali au kwa kutumia teknolojia, pia kuzijengea uwezo biashara, wajasiri amali, wabunifu na tabaka za ujuzi mbalimbali kupitia teknolojia.

Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, mpango huu utasaidia kuwa ni mwongozo muhimu kwa kuchochea mabadiliko ya kiuchumi Kenya kwa kutumia teknolojia.

“Kusudio ni kutengeneza muundo ili utuongoze wakati tukiendeleza juhudi za kutumia teknolojia hizi kwa mujibu wa mazingira yetu. Natumai nchi zote zinaona thamani ya kutumia muundo huu kwa ajili ya mazingira ya uchumi wa nchi zao ili waweze kufikia uwezo wao kamili wa mabadiliko ya kidigitali.

“Nchini Kenya, idadi ya matumizi ya Intaneti na manunuzi ya muda wa kuunganishwa yalifikia milioni 42.2 mwaka 2018, na mfumo wa matumizi ya broadband kwa ajili ya intaneti uliwafikia asilimia 45 ya idadi ya watu wote na takriban nchi nzima wameunganishwa kupitia mkongo wa taifa,” alisema.

Alisema hatua hii ni muhimu kwa Afrika, hasa ukizingatia kuwa Kenya ilichaguliwa na taasisi ya kimataifa Smart Africa Initiative, inayosimamia kuendeleza soko la pamoja la kidigitali Afrika, mwezi uliopita kutengeneza pendekezo la mpango wa uchumi wa kidigitali kwa ajili ya bara la Afrika

Rais Kenyatta alisema kwa kuzindua mpango wake, wa kwanza katika bara la Afrika, Kenya ilionyesha uwezo wa kufikia malengo ya kuwa kigezo kwa nchi nyingine za Afrika ambazo zimejiunga na safari hii ya mabadiliko ya kidigitali.

Mpango  huo umeonesha masuala mtambuka kama vile mifumo ya sheria na sera, teknolojia zinazoibuka na usimamizi wa data.

Rais Kenyatta amesema Kenya iko tayari kuchangia uzoefu wake na nchi nyingine, na pia iko tayari kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine.

Share.

About Author

Leave A Reply