Thursday, August 22

Profesa Kabudi awananga aliodai wanamuonea wivu, yeye anaitumikia nchi

0


By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema yeye ni mtu aliyesajiliwa katika dirisha dogo lakini hawezi kuyumbishwa na watu wasiomtakia mema.

Amesema hayo alipokuwa akijibu hoja za wabunge leo Alhamisi Mei 29,2019 bungeni Jijini Dodoma.

Amejisifu kuwa amekuwa turufu ya nchi kwa kutoa mchango mkubwa kwenye baadhi ya maeneo.

Waziri huyo ambaye ni mbobezi pia kwenye masuala ya sheria, amesema hasononeshwi wala hatishwi na kelele za watu kwa sababu uzalendo wake kwa Taifa hauna shaka.

Profesa Kabudi ametaja kazi alizowahi kuzifanya kabla ya kuwa serikalini ni pamoja na kuandika Sheria ya Mazingira ambayo inatumika hadi sasa.

Nyingine ni upatanisho aliofanya baina ya wabunge wapinzani chini ya Hamad Rashidi Mohamed na Dk Wilbrod Slaa wakati wa kutunga sheria ya kupambana na rushwa na amezisoma hansard (kumbukumbu rasmi)  za Bunge zilizomtaja kwa wakati huo.

“Anayemchukia Kabudi na aendelee kumchukia na anayempinga na aendelee kumpinga, lakini Kaburi atabaki yule yule siku zote,” amesema.

Waziri huyo amejilinganisha na Mtume Yusufu kwa waumini wa Kiislamu lakini kwa Wakristo akawaomba wakasome Biblia katika Kitabu cha Mwanzo kuhusu kisa cha Yusufu na nduguze akisema yeye ndiye Yusufu, hivyo wasimpeleke utumwani.

Amesema hii si mara yake ya kwanza kuitwa kwa ajili ya kufanya kazi ngumu ya nchi yake.

Akirudia rudia maneno yake ya usajili wa dirisha dogo huku akipigiwa makofi na wabunge, amegusia juu ya haki za binadamu huku akisema katika kesi ya wabunge wa Chadema, Ester Matiko (Tarime Mjini) na Freman Mbowe (Hai) kwamba alifuatwa mara kadhaa kutaka aingilie kati lakini alikataa.

Share.

About Author

Leave A Reply