Sunday, August 18

Polisi kukusanya Sh118.317 bilioni kwa makosa ya usalama barabarani

0


By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2019/20, Polisi inatarajia kukusanya Sh118.317 bilioni kwa makosa ya ukiukwaji wa usalama barabarani.

Hilo ni kadirio la jumla ya makosa 3.1 milioni ambayo wanalenga kuyakamata na kuyatoza faini kwa vyombo vya moto vitumiavyo barabarani.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mbunge wa Morogoro Kusini, Prosper Mbena, amesema ni vyema polisi ikajikita katika kutoa elimu zaidi kuliko kufikiri kukuza mapato kwani makosa hayo hupesababisha wakati mwingine vifo kwa Watanzania.

Mbena amesema sambamba na hilo, ni vyema Serikali ikakamilisha mchakato wa sheria ya usalama barabarani ambao umechukua muda mrefu kwani sheria hiyo itasaidia kupunguza makosa ya barabarani.

Ametaja kuwa kazi mojawapo kwa polisi ni kutoa elimu kabla ya kutoza faini kwa wakosaji ili waanze kwa kupunguza makosa yao.

Mbunge huyo amesema bado kuna shida ndani ya polisi kutokana na kutopewa fedha kwa wakati unaotakiwa hivyo kuchangia kuzorotesha shughuli zao.

Ameitaka Serikali kutoa fedha kwa wakati unaotakiwa kutokana na umuhimu wa polisi katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaimarika.

Share.

About Author

Leave A Reply