Friday, July 19

Polisi Dar waua washukiwa sita wa ujambazi, wakamata silaha ya kivita

0


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaua washukiwa sita wa ujambazi na kukamata silaha tatu aina ya AK47, risasi 11 na mabomu manane.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema mauaji hayo yamefanyika leo Alhamisi Novemba 29, 2018 maeneo ya Ubungo UFI, Dar es Salaam kupitia kikosi kazi maalum cha kupambana na ujambazi.

Amesema pamoja na silaha na risasi hizo, walifanikiwa kukamata kitambulisho chenye namba OP 0216239 chenye jina la Theophil Manirakiza mkazi wa Rukana Rugombo nchini Burundi na kitambulisho cha kazi kinachotumiwa na kikundi cha CNDD-FDD chenye jina hilo la Theopili Manirakiza.

Amesema majambazi hao waliuawa baada ya mtego uliowekwa na askari kufuatia taarifa za watuhumiwa watatu waliokuwa wamekamatwa (Willy [email protected] raia wa Burundi, Jean Mugisha raia wa Burudi na Mtanzania Omary Nassoro.)

Mambosasa amesema watuhumiwa hao waliokuwa na bunduki tatu aina ya AK47 na magazini 8, risasi 217 na mabomu ya kutupa kwa mkono manane, ambao walipanga Novemba 29, 2018 majira ya saa 10:30 alfajiri kufanya tukio la kumpora mfanyabiashara aliyekuwa akisafiri kwenda Morogoro akisadikiwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuwepo kwa matukio ya uhalifu yaliyotokea huko Mabibo External, Dar es Salaam Novemba 3, ambapo mfanyabiashara mmoja wa huduma za kifedha za simu aliporwa Sh50 milioni na huko Tegeta jijini humo Novemba 15, mfanyabiashara raia wa China ambaye aliporwa Sh10 milioni.

Kamanda huyo alisema jambazi Willy Irakozes alikuwa akitafutwa kwa kufanya matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa katika tukio la kuvamia Benki ya NMB Temeke, Dar es Salaam ambapo aliua askari wawili na raia.

“Machi 15, akiwa anashikiliwa kituo cha Polisi Kagongwa Kahama, Shinyanga kwa makosa mbalimbali yeye na wenzake walitoroka baada ya kuwaua askari polisi wawili na kutoroka na silaha mbili aina ya AK47,” amesema.

“Matukio mengine waliyoshiriki ni pamoja na kuteka mgodi wa Tulawaka Geita mwaka 2011, kuvamia maduka ya kubadilishia fedha za kigeni huko Zanzibar, mwaka 2012 walivamia kituo cha mafuta huko Kagera na kufanya mauaji,” ameongeza.

Katika matukio mengine, Kamanda Mambosasa amesema, “Walivamia maduka yaliyopo karibu na kituo cha Polisi Chato, Geita na hivyo kukishambulia kituo ili kurahisisha uporaji ambapo walipora Sh3 milioni na mwaka 2010 walivamia mgodi wa Nyamongo (Mara) na kufanya mauaji ya askari moja na kujeruhi wengine.”

 

Share.

About Author

Leave A Reply