Thursday, February 21

Pesa za Simba sc zinavyobadili taswira ya soka la Tanzania

0


By Charles Abel na Mwanahiba Richard

MAENDELEO ni jambo jema ambalo kila mmoja anapenda kuona likitokea lakini huwa halipatikani kwa wepesi wala njia za mkato.

Ni lazima safari au harakati za kupata mafanikio au maendeleo kwenye jamii au jambo fulani, zikutane na vigingi sambamba na nyakati ngumu ambazo yeyote aliyefanikiwa au mwenye kiu ya kufanikiwa ni lazima apite ili atimize lengo lake.

Maendeleo huwa hayaji kirahisi na ni lazima watu wakubali kuvuja machozi, jasho na damu vinginevyo wataishia njiani na kujikuta wakiishia kuwa mashuhuda wa mafanikio ya wenzao.

Bajeti ya Sh6 bilioni iliyotangazwa na Simba, Jumapili iliyopita kwa ajili ya msimu wa 2018/2019 kwa kiasi kikubwa inatoa taswira ya mageuzi ambayo yanakwenda kutokea katika soka la Tanzania.

Ingawa bajeti hiyo inaihusu Simba pekee, ina athari, pia inazigusa timu nyingine pamoja na soka la Tanzania kijumla na kivyovyote ni lazima zikabiliane na maisha mapya ambayo pengine hatukuwahi kuyaona hapo awali.

Kupanda thamani/mishahara ya wachezaji

Katika bajeti ya Simba msimu huu, wametenga kiasi cha Sh 700 milioni ambacho kitatumika kwa ajili ya usajili wa wachezaji. Tayari hadi sasa wametumia takribani Sh375 milioni kuwasajili wachezaji wanane katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa ambao ni Pascal Wawa, Hassan Dilunga, Mohammed Rashid, Adam Salamba, Cletous Chama, Deogratias Munishi, Marcel Kaheza na Meddie Kagere.

Kwa bajeti ya Sh700 milioni maana yake, Simba inaweza kusajili wachezaji takribani 10 kwa kumpa kila mmoja Sh70 milioni.

Hii inaziweka klabu nyingine kwenye wakati mgumu kwani nazo zitalazimika kuongeza mafungu yao ya usajili ili angalau ziweze kupata wachezaji washindani au wale wenye ubora mkubwa kwani vinginevyo kila mchezaji nyota akili yake ataielekeza mahali ambako ana uhakika wa kupata fungu kubwa la fedha.

Kupanda kwa gharama za uendeshaji klabu nyingine

Fikiria ni mchezaji wa klabu gani atakuwa tayari kupambana ili timu yake itwae ubingwa wa Ligi Kuu pasipo kupatiwa bonasi yoyote au kupewa fedha kiduchu, wakati wale wenzao wa Simba wakiwa na uhakika wa kuvuna Sh400 milioni mwishoni mwa msimu kwa kuchukua ubingwa wa ligi tu?

Fikiria ni mchezaji gani wa kikosi cha vijana cha klabu nyingine au timu ya wanawake atakubali kucheza huku bajeti ya timu ikiwa kiduchu halafu wakati huohuo Simba imetenga kiasi cha Sh35 milioni kwa ajili ya kikosi chao cha vijana na wanawake?

Ni mchezaji au kocha gani anayeweza kuwa na utulivu au kuwa na molali kwenye timu ambayo bajeti yake ya mishahara haifikii hata robo ya bajeti nzima ya Simba takribani Sh2.7 bilioni kwa ajili ya kulipa mishahara tu ya wachezaji na makocha?

Kivyovyote bajeti ya Sh 6 bilioni ambayo ilitangazwa na Simba, Jumapili iliyopita inazipa ulazima klabu nyingine kuingia katika maisha ya gharama kubwa zaidi tofauti na yale ambayo zilizoea kuishi hapo kabla vinginevyo zitajikuta zikiwa wasindikizaji huku zikiwa na vikosi ambavyo haviwezi kutoa ushindani mkubwa kwa Simba.

Simba hawakukurupuka kutangaza bajeti ya Sh6 bilioni kwa mwaka pasipokuwa na uhakika wa vyanzo vinavyoweza kuwapatia kiasi hicho cha fedha.

Kwa mujibu wa baejti hiyo iliyosomwa kwenye Mkutano Mkuu, fedha hizo zitapatikana kupitia mapato ya milangoni na wameweka makadirio ya kupata kiasi cha Sh870 milioni.

Mapato hayo ya milangoni ni yale ya mechi za Ligi Kuu, mechi za kirafiki na Simba Day huku wakitarajia kuvuna kiasi cha Sh1.7 bilioni kutokana na mikataba ya udhamini binafsi na ile ya Ligi Kuu.

Mikataba hiyo ni ya Kampuni za SportPesa, Azam Media, KCB Bank, A One Products, MO Assurance na Raha Internet na kiasi cha takribani 435 wakitarajia kupata kutoka kwenye haki za matangazo ya runinga.

Fedha za zawadi za mashindano ya SportPesa Super Cup na Kombe la Kagame zimeiingizia timu hiyo kiasi cha Sh95.7 milioni huku kiasi cha zaidi ya Sh4.98 bilioni wakitarajia kuvuna kutoka kwenye mapato ya mauzo ya jezi, tozo ya majengo, ada za wanachama, mkopo kutoka Kampuni ya METL na kadhalika.

Simba wamepanga bajeti hiyo ya Sh6 bilioni itumike kugharimia huduma na masuala mbalimbali ambapo gharama za timu kijumla ni kiasi cha Sh5.1 bilioni, kiasi cha zaidi ya Sh658 milioni kikitumika kwa shughuli za kiutawala wakati takribani Sh233 milioni zikitengwa kugharamia ujezi wa miundombinu ya klabu hiyo.

Share.

About Author

Leave A Reply