Sunday, August 25

Padri azungumzia wanaojinyonga

0


By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mke wa Rais wa Tanzania, Janeth Magufuli ameungana na mamia ya waumini kushiriki ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam leo Aprili 19, 2019.

Ibada hiyo iliyoongozwa na Padri Paul Haule ni tafakari ya mateso ya Yesu Kristo ambaye aliuawa miaka 2000 iliyopita na kukumbukwa na wakristo duniani kama alama ya ukombozi.

Katika mahubiri yake, Padri Haule amewataka waumini wasijinyonge wanapofikwa na magumu katika maisha bali watubu na kumrudia Mungu kwa sababu anasamehe.

“Katika maisha yetu, tuwatumie Petro na Yuda kama funzo kwetu. Wote walimsaliti Yesu lakini Petro aliomba msamaha lakini Yuda alijinyonga. Kwa hiyo, tuwe kama Petro, tukikosea tutubu, Mungu anasamehe,” amesema.

Padri Haule amesema mateso ya Yesu ni kielelezo cha ukombozi wa binadamu kwa sababu alijitoa sadaka kuwakomboa wanadamu ikiwa ni sadaka ya upatanisho. Amesema mateso bila upendo mwisho wake ni Jehanamu.

“Mateso ukijumlisha na upendo ni sawasawa na sadaka. Mateso bila upendo hiyo siyo sadaka. Yesu alijitoa sadaka, mateso yale msalabani yatufariji katika maisha yetu ya kila siku,” amesema.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamesema Ijumaa Kuu inawapa nafasi ya kutafakari maisha yao na uhusiano wao na Mwenyezi Mungu kila siku.

“Hii ni siku muhimu sana katika imani yetu, tunakumbuka mateso na kifo cha Bwana Yesu ambaye tunaamini kupitia yeye ndiyo tulipata ukombozi,” amesema Chrispin Massawe, muumini wa kanisa hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply