Friday, July 19

Padre Magala kukaimu nafasi ya Askofu Chengula

0


Mbeya.  Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Marek Solczynsk amemtangaza Padre Francis Magala kuwa msimamizi wa kanisa hilo Jimbo la Mbeya hadi pale atakapopatikana mrithi wa aliyekuwa askofu wa jimbo hilo, Evarist Chengula.

Balozi Askofu Solczynsk alimtangaza Padre Magala jana Jumanne Novemba 27, 2018 baada ya kumalizika kwa misa ya mazishi ya Askofu Chengula iliyofanyikia Kanisa la Bikira Maria wa Fatma Parokia ya Mwanjelwa Jijini Mbeya.

Kabla ya kutangazwa kwa Padre Magala, Askofu Mkuu Jimbo la Songea, Damian Dalu  alisema baada ya Askofu Chengula kufariki Novemba 21, 2018 kulifanyika kikao kwa mujibu wa sheria za kanisa hilo ili kumpata mtu sahihi atakayekuwa msimamizi wa jimbo hilo hadi pale atakapopatikana askofu mwingine.

“Tukiongozwa na sheria ya kanisa namba 432 hadi namba 436, ikatuongoza kwamba turudi kwenye taratibu za kutazama wenye sifa za mmoja ambaye  anaweza akawa ni msimamizi wa jimbo baada ya askofu kufariki.

“Kwa hiyo tulizingatia vifungu vinavyohusika katika sheria za kanisa, hatua kwa hatua na mchakato huu ulifanyika Novemba 23, 2018 na washauri walioketi kutafuta jina hilo wakatoka na jina moja la ambaye atakaa hapo hadi pale atakapopatikana  askofu wa jimbo,” alisema Askofu  Dalu.

Baada ya Askofu Dalu kuelezea mchakato mzima ulivyofanyika hadi kupata jina la padre aliyepatikana na kikao cha wajumbe waliokaa kuchagua kupata msimamizi wa jimbo hilo, akamkaribisha Balozi Askofu Solczynsk na kumtangaza Padre Magala.

“Ninamtangaza Padre Francis Magala kuwa msimamizi wa Jimbo la Mbeya hadi pale atakapopatikana askofu wa jimbo hili,” alisema.

Awali, Padre Magala alikuwa makamu askofu wa jimbo hilo kabla ya kifo cha Askofu Chengula na ndiye aliyesoma wasifu wa marehemu kwa umakini wakati wa misa hiyo.

Akisoma wasifu huo, Padre Magala alimtaja Askofu Chengula kwamba alikuwa ni kiongozi aliyesimamia maono na misimamo yake katika kipindi chote cha utawala wake.

Alisema Askofu Chengula alianza kazi yake ya uaskofu akiwa na kauli mbiu yake ya ‘Mungu Dira Yangu’, kauli mbiu ambayo ilijidhihirisha na kuonekana katika kazi zake zote za kiuchungaji alizotenda jimboni hapo.

Share.

About Author

Leave A Reply