Sunday, August 18

Nyoka wawili wamfurusha George Weah ofisini

0


Nyoka wawili wameibuka katika ofisi ya Rais wa Liberia, George Weah, hatua iliyomshinikiza kuikimbia ofisi hiyo na kufanya kazi katika ofisi binafsi.

Ofisa habari, Smith Toby amenukuliwa na BBC akisema kwamba Jumatano iliyopita nyoka wawili weusi walipatikana katika ofisi ya wizara ya masuala ya kigeni.

“Wafanyakazi wote wametakiwa kutoingia katika ofisi hiyo ili kupiga dawa kuhakikisha kuwa wadudu wote wanaotambaa na kutembea wanaangamizwa katika jumba hilo,” alisema Toby.

”Wizara ya masuala ya kigeni ndimo iliko ofisi ya rais. Hivyo basi, wizara ikalazimika kuandika barua ikiwasihi wafanyakazi kusalia nyumbani huku ikiendelea kuweka dawa hiyo,” alisema.

Kanda ya video iliyochapishwa katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la African News ilionyesha wafanyakazi wakijaribu kuwashambulia nyoka wakati walipoonekana katika eneo la kukaribisha wageni kwenye jengo hilo.

”Nyoka hao hawakuuliwa,” Toby alisema. ”Kulikuwa na shimo mahali fulani ambalo walikimbilia”.

Maofisa wa polisi na maofisa wa usalama wa rais walionekana wakiyalinda makao ya Weah katika mji mkuu wa Monrovia.

Msafara wa magari wa rais huyo ulionekana umeegeshwa nje ya jumba hilo.

Toby alisema kuwa wizara ya masuala ya kigeni ilianza kunyunyiza dawa hiyo siku ya Ijumaa.

”Jumba hilo limekuwa katika eneo hilo kwa miaka kadhaa sasa kwa sababu ya mfumo wa maji taka, hivyo basi kuna uwezekano wa nyoka kuingia katika jumba hilo,” alisema.

“Rais anarudi katika ofisi yake rasmi siku ya Jumatatu baada ya dawa hiyo kunyunyizwa bila kujali iwapo nyoka hao watapatikana na kuuawa au la,” alisema.

Share.

About Author

Leave A Reply