Thursday, August 22

Niyonzima, Okwi, Tambwe wabinafsisha ubingwa Ligi Kuu Bara

0


By OLIPA ASSA na ELIA SOLOMONI

Dar es Salaam. KIPINDI Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) liliporuhusu klabu kusajili nyota 10 wa kigeni na kutoa ruksa wote kutumika katika mchezo mmoja, kuna baadhi ya wadau walichonga sana na kuona wingi wa wageni wala si ishu sana.

Lakini, buana kumbe ujio wa mapro wa kigeni umeletea tija kutokana na baadhi yao kuzibeba klabu zao, ambapo Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe wamefunika mbaya katika orodha ya wageni waliowahi kucheza soka nchini.

Unaambiwa nyota hao wa Simba na Yanga wamefunika kwa kutwaa mataji mengi katika Ligi Kuu Bara, kinara wao akiwa kiungo fundi wa mpira, yaani Niyonzima.

Rekodi zinaonyesha Niyonzima ametwaa mataji sita mpaka sasa, mawili akiwa na Simba na manne alipokuwa Jangwani kuanzia mwaka 2011-2019.

Mnyarwanda huyo ametwaa matano mfululizo kuanzia 2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017 akiwa na Yanga na mawili ya msimu wa 2017-2018 na msimu huu akiwa na Simba.

Licha ya kutopata nafasi kubwa kuitumukia Simba msimu uliopita na hata mwanzoni mwa msimu huu kutokana na majeruhi, lakini Niyonzima ametisha, kwani hata Tambwe anayekipiga Yanga ametwaa mara tatu mfululizo taji hilo akiwa na timu hiyo.

Tambwe amelibeba taji hilo katika misimu ya 2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017, huku Okwi akitwaa mara nne akiwa na Simba, msimu wa 2009-2010, 2011-2012, 2017-2018 na 2018-2019 tangu aanze kucheza ligi kwa mara ya kwanza 2010 mpaka 2013.

Okwi amekuwa akiondoka na kurejea Simba kwani msimu wa 2013 aliondoka kwenda Etoile du Sahel ya Tunisi ambapo hakufanikiwa kukaa kwa muda mrefu msimu 2013-2014 alijiunga na Yanga, lakini baadaye akarejea Simba 2014-2015.

Mwaka 2015 mpaka 2017 alikuwa na klabu ya SønderjyskE, baadae akarejea SC Villa ambapo mwaka 2017 alirudi tena Simba na kufanikiwa kuchukua ubingwa mara mbili.

Kiungo huyo ambaye ameifungia Simba mabao mawili katika Ligi Kuu tangu ajiunge nayo akitokea Yanga msimu uliopita alisema;

“Nimeishi vizuri Tanzania na najivunia mafanikio niliyopata, siwezi kusema mimi ni bora kuliko wengine, ila ni mapenzi ya Mungu, nikiwa Yanga nilijitahidi kucheza kwa uwezo wangu ili kuisaidia klabu.”

“Nashukuru Mungu kwa sababu nilikuwa na maisha mazuri Yanga, lakini kama unavyojua maisha ya mpira ni safari, nikajiunga na Simba ambako nilikuwa nikusumbilia na majeraha.

“Najiona mwenye bahati na katika hali yangu ya kawaida kwa sasa na naufurahia mpira na naona fahari kushinda ubingwa wa ligi mara tano mfululizo.”

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema Okwi, Niyonzima na Tambwe ni mastaa wa mfano wa kuigwa wakiwa kwenye viwango vyao na ni chachu kwa wazawa.

“Unapomzungumzia Niyonzima, Okwi na Tambwe hakuna asiyejua mchango wao, wana uwezo na akili ya mpira hata mafanikio ya mataji hayo wanastahili”alisema.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Yusuf ‘Tigana’ alisema; “Kwa ambavyo timu hizo haziwezi kukaa na wachezaji kwa muda hususani wale wasio na uwezo, hivyo Okwi, Niyonzima na Tambwe wana uwezo wa kuwafanya wadumu nazo kwa muda mrefu.”


Share.

About Author

Leave A Reply