Sunday, August 25

NDIO HIVYO, Liverpool inapitia bonde la mauti

0


ULE mstari katika biblia unaosema ‘bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu…nitembeapo bonde la mauti…yeye ndiye hunichunga..’. kitu kama hicho. Nakiona pale Anfield.

Mpira mchezo wa ajabu. Nilikuwa namsikiliza Paul Scholes mahala. Alikuwa akiwashambulia mastaa wa Manchester United. Ilikuwa ni kabla ya pambano la Jumatano dhidi ya wapinzani wao Manchester City. Alidai ingekuwa upuuzi kwao kufungwa na Everton halafu wakakaza dhidi ya City na kushinda mechi hiyo kwa gharama za kuipa ubingwa Liverpool.

Kauli za hivi zinaashiria kitu. Scholes na wahafidhina wa Old Trafford wanaona bora City wachukue ubingwa kuliko Liverpool. Sir Alex Ferguson aliwahi kuwaita City majirani wenye kelele. Lakini bado wahafidhina wa Old Trafford wanaona bora majirani wenye kelele kuliko Liverpool.

Kisa? Manchester United ina mataji 20. Liverpool wana mataji 18. Wanajua Liverpool wakichukua ubingwa watabakiza taji moja tu wawafikie. Kama Liverpool hii ikichukua kombe, basi inaweza kuchukua tena na tena kwa sababu wana kikosi imara.

Katika wachezaji wa Liverpool wanaotamba sasa, mchezaji mzee anaweza kuwa James Milner. Wengine waliobaki wana umri wa kusumbua tena na tena. Kama wakichukua ubingwa ina maana watawadhibiti wachezaji wao wasihame kwenda Real Madrid au Barcelona.

Katika miaka ya karibuni Liverpool imewapoteza Fernando Torres, Luis Suarez, Philippe Coutinho na Raheem Sterling kwa kisingizio walikuwa wanataka kwenda kucheza katika klabu ambazo zina uhakika wa kutwaa mataji.

Kina Mohamed Salah na Sadio Mane nao wanaweza kufuata njia hii kama wakiona mabao yao hayazalishi mataji.

Lakini kama wakichukua taji hili watabakia na kuifanya Liverpool kuwa kubwa kuliko ilivyo. Hawatachukua mara moja. Watachukua tena na tena. Kwa umri walionao wanaweza kufikisha mataji 20 na kisha kuchukua zaidi na kuiweka United chini.

Haya yote yanatokea wakati Ferguson hayupo tena Manchester United na wanapitia nyakati za tabu. Hawajauona ubingwa wa England kwa mwaka wa sita sasa.

Si tu kwamba hawajaona, lakini hawana matumaini ya kuuona mwakani. Kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer juzi amekiri hilo.

Kama Manchester City ikichukua basi haiwezi kuwa tatizo kwa Manchester United. Litakuwa taji lao la sita katika ligi na bado wana safari ndefu ya kuifikia United yenye mataji 20. Ndio maana haiwasumbuia sana mashabiki wa United kuona City anachukua.

Chuki ya United dhidi ya Liverpool inaeleweka. Chuki za wengine dhidi ya Liverpool? hizi nazo zinaweza kueleweka ingawa sababu zao hazina uzito ule ule kama wa mashabiki wa Manchester United na akina Paul Scholes.

Kuanzia Hongkong, Texas, Mombasa, Cape Verde, Newala, Tokyo na kwingineko, mashabiki wa timu nyingine wamejumuika na mashabiki wa United kuiombea mabaya Liverpool wasichukue ubingwa wa England. sababu ni rahisi tu. City hawatasumbua wengine.

Kuna mashabiki wachache wa Manchester City mitaani. Ni ngumu kukutana na mashabiki wa Manchester City ambao watakusumbua nyumbani, ofisini au mitaani. Wa Liverpool wapo wengi na watasumbua kweli kweli. Watu wanaliogopa jambo hili.

Mashabiki wa Liverpool wana majivuno na mpira. Wanajiona wao ndio wanaufahamu mpira. Wanaona wao ndio wameanza kupenda soka la Uingereza kabla ya mashabiki wa timu nyingine. Kwa England kwenyewe hali sio hii, kwa dunia nyingine nje ya England dunia ipo hivi na ndio maana mashabiki wa United, Chelsea na Arsenal wanajiuliza, itakuaje Liverpool wakichukua ubingwa wa England?

Sasa Liverpool inatembea katika bonde la mauti. Maadui ni wengi kando yao. Wanachungwa na Mungu tu. Ukitazama jinsi watu walivyoshangilia mabao ya City dhidi ya United ndio utagundua kwamba Liverpool wapo katika bonde la mauti.

Kitakachofurahisha ni kama wakichukua ubingwa huu. jinsi watakavyotamba. Jinsi ambavyo watastahili kutamba. Kwanza ni kwa sababu watakuwa wamerudisha heshima yao iliyopotea kwa miaka 29.

Pia ni jinsi walivyoweza kuvuka katika bonde la mauti. Hakuna timu ambayo itakuwa imechukua ubingwa katika mazingira magumu kama wao.

Jaribu kuwafikiria Leicester City. Ulikuwa ubingwa wao wa kwanza lakini watu walisafiri nao kwa upendo. Mashabiki wa Manchester United. Manchester City, Liverpool, Chelsea, Arsenal na wengineo kote duniani walipenda walichokiona kutoka kwa Leicester. Wakati wakikaribia kutimiza ndoto yao hawakupita katika bonde la mauti. Wengi walipenda wachukue.

Kwa kadri ninavyoona, siku hizi timu ambazo zina raha na hazisakamwi sana zinapotaka kuchukua ubingwa ni hizi ambazo hazina mashabiki wengi mitaani kama Manchester City na Leicester City. Zile zenye mashabiki wengi zinakupitisha katika bonde la mauti. Ndicho kinachotokea kwa Liverpool. ndicho kitakachotokea kwa timu nyingine kama Arsenal, Chelsea, na Manchester United zikigombea ubingwa na City. Hawawezi kuachwa salama. Wataandamwa. Watu wataungana kuwaandama.

Share.

About Author

Leave A Reply