Tuesday, July 23

NDANI YA BOKSI: La Wasafi, Kiba kashituka usingizini… Deal done!

0


Madogo wamekunjua roho, kiroho safi. Walichofanya ni kuwatazama wafuasi wao. Wakajiuliza tunataka nini? Pesa. Sasa tunasubiri nini zaidi? Hakuna. Ebo! Mtaji mkubwa katika uso wa dunia hii ni watu. Watu ndo kila kitu. Dai na Kiba wana watu.

Dai alitazama kulia akageuka kushoto. Akarusha macho mbele na nyuma. Hakumuona mama la mama Zari wala bebe la bebe Hamisa. Wema? Hapana, wakati wake umepitwa na wakati. Nani sasa wa ‘kutrend’ na Wasafi Festival, kipindi ambacho kelele za ushoga zikiwa zimetawala?

Mara ‘Konki Masta’ kazua la kulizua. Dangote hakupoteza muda. Dudubaya kasainishwa kuwa mmoja wa watumbuizaji kwenye Wasafi Festival. Siku hizi bila kupata ‘trend’ ya kutosha mitandaoni biashara ya burudani itakuua kwa presha. Hapa ‘Konki Masta’ hakwepeki.

Kitendo cha Diamond kutangaza uwepo wa ‘Konk Masta’, Instagram ilichafuka vibaya sana. Dudubaya kaiteka kwa sasa na Wasafi Festival ikaanza kusambaa vinywani, machoni na vichwani mwa watu. Bao la kwanza kwa Diamond katika kutangaza shughuli yake.

Katumia ‘kiki’ ya ‘Konki Masta’ kumuingiza na Kiba kijanja: “Kuna wasanii hawapewi nafasi kwenye shoo kubwa kwa sababu hawajatoa wimbo mwaka huu. Lakini wana watu, ndiyo Dudubaya. Nilikuwa namtazama jukwaani kabla sijatoka, ni faraja kwangu kupanda naye jukwaa moja.” Kauli ya kibiashara.

Ni kama anatongoza demu vile na asipindue, akaendelea: “Pia ningetamani sana kakaangu Ali (Kiba) awepo na kupanda naye jukwaa moja, lengo ni kuukuza muziki wetu ili mataifa mengine kama Wanijeria wajue sisi ni nani.” Kiba angeanzaje kupotezea ushawishi wa adabu kutoka kwa ‘Brazamen huyu’? Dangote ana watu wengi, pia Kiba ana watu. Anaachaje pesa ya maelfu ya wafuasi wa King Kiba? Diamond akitumia lugha nyenyekevu, tulivu na laghai kama Wabunge kwenye kampeni. Mbele ya kamera za wanahabari kibao akaomba sana Kiba awepo. Mashabiki wa Kiba jeuri sana lazima ujishushe ili kuwanasa.

Hakuhitaji mabango wala posters za Wasafi Festival kujitangaza zaidi. Namna video ilivyosambaa mitandaoni ikimuonesha akiomba uwepo wa Kiba, ‘trend’ yake ni tangazo tosha. Kila kurasa mitandaoni ziliruka na video hiyo. Mjadala juu ya ombi hilo likawa bao la pili kwa Diamond na timu yake.

Matokeo yake stori ikawa ni ‘Konki Masta’ kupanda jukwaa la Wasafi Festival. Na Diamond kubembeleza Kiba awepo. Watu wakasahau ya ‘Konki Masta’ na Mange. Wakasubiri jibu la Kiba kwa Diamond. Kurasa nyingi mitandaoni zilijadili juu ya nini atajibu Kiba? Kitendo hicho kikawa bao la tatu kwa Dai na timu yake.

Lengo la Diamond ni Wasafi Festival ianze kuongelewa mitandaoni na mitaani (kutrend). Bila ‘Konki Masta’ na Alikiba ingekuwa ngumu. Watu walikuwa ‘bize’ na ‘Konki Masta’ na Mange. Kawapasua katikati na kufanikiwa kuua ‘trend’ yao. Akili kubwa hufanya kazi ngumu kuwa nyepesi.

Kiba ni akili kubwa nyingine. Diamond aliamini kuomba Kiba awepo kwenye shoo zake ingemsaidia kibiashara. Ni kweli, lakini kinyume chake, inaonesha Kiba muda mrefu alikuwa anatafuta jukwaa kubwa la kutangaza bidhaa yake. Wasafi wamekuja wakati muafaka na ni jukwaa sahihi zaidi kibiashara kwa Kiba.

Ni kama mwembe kuota Jangwani namna Wasafi walivyorahisisha ‘promo’ ya kinywaji cha Kiba. Anaanzaje kupuuza nyomi la wafuasi wa WCB? Kutoshiriki angeharibu, kushiriki kama msanii pia ingemshusha. Kakosa muda wa kushiriki kisanii, anashiriki kama mdhamini. Hili ni bao kubwa kwa Kiba. Yawezekana bila uwepo wa Wasafi Festival, asingepata jukwaa kubwa na zuri zaidi la kutangaza kinywaji chake. Mpaka hapa siyo Diamond wala Kiba, kwa mara ya kwanza wamenufaika na jasho lao pamoja. Kulumbana kwa sasa bila kuingiza pesa ni ubwege kama ubwege mwingine.

Ingekuwa mbaya kama Kiba angekataa. Kukubali kwa kudhamini ni heshima kwa muziki na mashabiki na fursa kubwa kwake kibiashara. Diamond anawahitaji watu wa Kiba kwenye shoo zake. Kiba anawahitaji watu wa WCB kwenye kinywaji chake. Wameungana kuzitafuna pesa za mtaji wa watu walionao.

Kama Kiba asingejibu lolote, ‘ingeback fire’ kwake. Watu wasio na ‘utimu’ wangeona Kiba ni tatizo. Pia, Diamond asingemuomba Kiba awepo lingekuwa tatizo kwake. Na isingekuwa na maana kusema dunia itujue kimuziki. Diamond anamuhitaji sana Kiba. Kwa sababu yupo kwenye eneo pana zaidi ambalo atake asitake watu wa Kiba anawahitaji.

Kumtenga Kiba ni kujinyima wasikilizaji na watazamaji zaidi wa Wasafi FM na TV. Ni kupunguza nyomi la Wasafi Festival. Na kwa Kiba pia, siyo wakati wa kutambiana kwa nyimbo, wameshakuwa wafanyabiashara wakubwa wa bidhaa zinazohitaji kupata walaji wa kutosha. Anaweza kudhamini na vipindi Wasafi TV/radio.

Hili ni ganda la ndizi yaani mtelezo tu kwa Kiba. Watu wake wa masoko watakula pesa ya bure. Akili ya kuwaza wafanyeje ‘kupromoti’ bidhaa yao, Dai kawarahisishia. Lakini pia Dai kafaidika kwa ongezeko la wadhamini kwenye shoo zake. Mungu awape nini hawa madogo, gunia la chawa?

Hawa ‘mabishoo’ wa Tabata na Madale, wameteka kila kitu. Jamii inawaza na kujadili mambo yao kuliko maisha mengine. Tumesahau kuhusu Mo. Tumepuuza sakata la mashoga. Tunawajadili wao na biashara zao. Wakifa masikini yatakuwa maajabu makubwa zaidi kwa kizazi cha sasa.

Kwa Diamond siyo jambo la ajabu pale anapotaka pesa. Anaweza kufanya lolote ili jambo lake liende. Kwenye hili ni Kiba aliyeshituka usingizini na kutambua kuwa anaweza kuingiza pesa zaidi akifanya jambo na Diamond. Kiba ni jeuri hata mbele ya pesa, lakini kwenye hili ujeuri kaweka kando.

Tunawajua Team Kiba na Wasafi. Kiba angeshiriki kisanii mashabiki wake wangeumia kuonekana ‘The Big Boss’ anafanyishwa kazi na ‘Big Boss’ wa wapinzani wao. Ndiyo maana leo wanadiriki kusema ameanza na kudhamini shoo kesho atainunua na brand ya Wasafi yote.

Waacheni madogo wapige hela. Hata hao matajiri wa hizi kazi walianza kupiga pesa katika umri huu walionao. Kinachoendelea kwa Dai na Kiba ni matokeo ya kuzungukwa na watu sahihi. Aslay na wenzake wasome mchezo ili tuendelee kutengeneza matajiri na siyo dhiki kwenye muziki.

Share.

About Author

Leave A Reply