Thursday, February 21

Nanai wa MCL ateuliwa mjumbe wa bodi ya TECC

0


 Katika kutambua mchango wa uendelezaji ujasiriamali nchini, Serikali imemteua mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai kuwa mjumbe wa taasisi ya Ujasiriamali na Ushindani (TECC).

Pia, Serikali imezitaka halmashauri za miji na manispaa nchini kutenga maeneo ya viwanda na kuweka miundombinu itakayowavutia wajasiriamali na wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vidogvidogo, vya kati na vikubwa.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Walemavu), Stella Ikupa alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es as Salaam akizindua bodi mpya ya wadhamini wa taasisi hiyo.

Ikupa alisema maeneo hayo yakitengwa yatakuwa chachu kwa vijana kupata sehemu ya kufanyia ujasiriamali na wawekezaji kuwekeza katika viwanda.

Uzinduzi huo umekuja baada ya waasisi wa TECC kupata bodi mpya ya wadhamini na kuikabidhi majukumu ya kusimamia menejimenti ili iweze kufikia malengo yake ya kukuza ujasiriamali.

Wajumbe wapya wa bodi hiyo ni Profesa Burton Mwamila, Nanai, Sophia Mbeyela, Edward Furaha na Jennifer Bash huku mwenyekiti akiwa ni Bengi Issa.

Kwa upande wake Bengi alisema bodi hiyo ina wajumbe watano na itakaa madarakani miaka mitano.

Bengi alisema taasisi hiyo inajishughulisha na mambo ya ujasiriamali na ushindani nchini hasa kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kwenda shule na wanaotoka katika familia maskini.

Taasisi hiyo inashirikiana na wadau wakiwamo taasisi ya Kimataifa ya Kuendeleza Biashara (IYF); Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (Sido); Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF).

Naye meneja malezi, Daniel Mghwira alisema menejimenti na wadau wake wote watashirikiana na bodi hiyo kuhakikisha shughuli za kukuza ujasiriamali hasa kwa vijana zinapiga hatua.

Share.

About Author

Leave A Reply