Friday, April 19

Mwigulu kigogo wa 11 kunusurika kifo katika ajali

0


By Bakari Kiango na Rachel Chibwete [email protected]

Dar es Salaam/Dodoma. Tangu Machi 29 mwaka jana hadi Februari13, mawaziri wawili na wabunge tisa wamenusurika vifo kutokana na ajali za barabarani wakiwa safarini katika maeneo tofauti nchini.

Idadi hiyo imefikiwa jana baada ya mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba kunusurika kifo katika ajali aliyoipata akiwa Iringa.

Dk Mwigulu aliyewahi kuwa waziri katika wizara za Mambo ya Ndani na Kilimo, alipata ajali hiyo asubuhi katika eneo la Migori akielekea Singida kuhudhuria kikao cha kamati ya siasa cha mkoa.

Mbunge huyo ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, aliwaambia wanahabari waliomtembelea hospitalini hapo kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari lake kugonga punda waliokuwa wakikatisha barabara.

“Sikuwa naangalia mbele kwa sababu nilikuwa naongea na simu. Lakini ghafla nilishtushwa na tahadhari ya ajali niliyopewa na dareva wangu na nilipoangalia mbele niliwaona punda watatu wakikatisha barabara mmoja alifanikiwa kuvuka lakini wawili waligongwa,” alisema Dk Mwigulu.

“Nilichosikia ni sauti ya kishindo kikubwa kilichoashiria kuwa tumepata ajali.Tunamshukuru Mungu ni mwema na ametuepusha na kifo.”

Baada ya kishindo hicho, Dk Mwigulu alisema aliona moshi mkubwa umetanda ndani ya gari hali iliyoashiria kuwa chombo hicho cha usafiri kingeweza kulipuka muda wowote lakini wasamaria walifika na kuwaokoa kisha kuwapeleka hospitali.

Dk Mwigulu, katika ajali hiyo alikuwa yeye na dereva wake lakini mwenzake huyo alitoka salama.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika alisema mbunge huyo alifikishwa hospitalini hapo, akilalamikia maumivu makali kifuani, nyonga na mguu. Hata hivyo, alisema baada ya kumfanyia vipimo vya CT Scan, Ultra-sound na X- ray hakukuwa na mfupa uliovunjika.

Ajali hiyo ya Dk Mwigulu inaongeza idadi ya wabunge wakiwamo mawaziri kupata misukosuko barabarani. Kabla ya Mwigulu, Februari 10, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Zainab Mussa alipata ajali akiwa Dumila, Morogoro akitokea Dodoma.

Kabla ya ajali hiyo, Novemba 11 mwaka jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipata ajali eneo la Iguguno, Singida baada ya gari lake lililokuwa na watu saba kupinduka mara nne wakati akielekea mkoani Dodoma.

Septemba 24, mwaka jana, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alipata ajali katika Kijiji cha Kibutuka akiwa safarini kuelekea Liwale kushiriki kikao cha kamati ya siasa ya Mkoa wa Lindi.

Kiongozi mwingine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalah ambaye alipata ajali Agosti 4, mwaka jana huko Magugu, Manyara iliyosababisha kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba.

Mbali na hao, Machi 29, mwaka jana, wabunge sita kutoka Zanzibar, Haji Ameir Haji (Makunduchi), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni), Bhagwanji Meisuria (Chwaka), Makame Mashaka Foum (Kijini) na Juma Othman Hija (Tumbatu), walipata ajali katika eneo la Bwawani mkoani Morogoro wakitokea Dodoma.

Share.

About Author

Leave A Reply