Tuesday, August 20

MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA : Wadau waidadavua sekta ya kilimo ndani nje

0


By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wadau wa kilimo wameeleza ili sekta hiyo ifanikiwe na kuleta matokeo chanya nchini, lazima zichukuliwe hatua madhubuti kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.

Changamoto hizo ni pamoja na utitiri wa kodi, upatikanaji mitaji, masoko, mabadiliko ya sera yasiyotabirika, miundombinu, pamoja na kutokuwepo kwa mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji.

Hayo yalielezwa juzi wakati wa kongamano la Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na kampuni ya Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL) likiwa limebeba kauli mbiu ya ‘Kilimo, Maisha yetu.’

Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa huru la Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema miongoni mwa vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi ili kuimarisha sekta ya kilimo ni pamoja na kuwa na mazingira rafiki ya kisera, kodi na taasisi zinazosimamia sekta hiyo.

Alisema kwa sasa kuna utitiri wa taasisi za kusimamia sekta ya kilimo jambo linalowakatisha tamaa wakulima na wawekezaji. “Tuna taasisi, kama unataka kuwekeza kwenye maziwa unahitaji kujisajili kwa taasisi hadi 26. Tutumie teknolojia ili ikiwezekana wajisajili mitandaoni,” alisema Rukonge.

Pia, aligusia suala la huduma rafiki kwa mwekezaji, miundombinu pamoja na kodi hasa kwa wawekezaji wa ndani ambao hutengeneza ajira nyingi.

Rukonge alisisitiza kuwa ipo haja ya kuwa na sera zinazotabirika ili kuhamasisha uwekezaji na ukamilishaji wa miradi.

Jambo lingine lililozungumziwa ni kukosekana miundombinu ya uhifadhi mazao yanayozalishwa, hali inayosababisha kuharibika.

Rukonge alisema kwamba kati ya asilimia 35-40 ya mazao ya nafaka hupotea baada ya kuvunwa, huku asilimia 60 ya matunda na mboga yanaharibika, hivyo akashauri kuimarishwa teknolojia ili kuepusha hasara.

Hoja hiyo pia ilizungumzwa na Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Kilimo Tanzania, Timothy Mmbaga aliyesema kabla ya kufanya uzalishaji wa mazao ni vyema kuangalia miundombinu ya uhifadhi wa chakula iliyopo kama inaweza kukidhi kiasi kitakachozalishwa.

Alisema kutokana na kutokuwapo kwa miundombinu rafiki, wazalishaji huzalisha kile kinachotosha kuuza na si kwa ajili ya kutunza.

“Hata ukiangalia wale wanaolima bidhaa za matunda na mbogamboga hakuna ‘Cold Chain’ iliyoandaliwa kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao. Licha ya kuwa sehemu hiyo ina fursa kubwa lakini miundombinu ni changamoto kubwa.”

“Endapo tutaweza kutengeneza miundombinu bora itakuwa fursa kwetu ya kuhifadhi chakula kingi kinachoweza kufikia tani 500,000 hizi hata njaa ipige kwa miaka 4 sisi tutakuwa hatuna wasiwasi, sekta binafsi mnanafasi ya kuwekeza katika upande huu.”

Mtafiti wa Kilimo wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Dk Anna Temu alisema kuna haja ya kuangalia kwa undani suala la masoko.

Alitaja masoko hayo kuwa ni ardhi, rasilimali watu, teknolojia na huduma za ugani akisema yakitiliwa mkazo, kilimo kitafanikiwa.

“Kuna haja ya kuangalia soko la rasilimali watu, lazima tujue vijana tulioanao uwezo wao kwenda kwenye kilimo. Soko la wajasiriamali watu tulionao hawawezi kuwafikia wakulima kwa ufanisi,” alisema.

Akizungumzia mitaji, Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine alisema zipo fedha kwa ajili ya kuwakopesha watu wenye nia ya kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

Alisema ipo fursa ya mabenki kuendelea kutoa fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo kinachotakiwa ni kwa wahusika kutengeneza mawazo ya miradi yenye tija.

Alisema benki hiyo kwa kushirikiana na nyingine, wametenga Sh80 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima wadogo

“Sasa hivi hakuna tatizo la kupata mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya kufanikisha miradi ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na tunataka wigo wa mabenki kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo uongezeke,” alisema

“Wapo wengi wanauza bidhaa zao masoko ya nje tena kwa kuzingatia vigezo vyote, kwa nini wanashindwa kufuata vigezo vinavyohitajika kwa soko la ndani ili waziuzie hoteli zetu,” alisema

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema ipo fursa kubwa kwenye kilimo na kuwataka wananchi na wadau kuwekeza upande huo.

Alisema kuna uwanja mkubwa kwa wakulima waweze kupata mafanikio huku akisisitiza kuwa kuna fursa kubwa kwenye kilimo cha mazao ya kimkakati mfano maparachichi na michikichi.

Mambo aliyotaja ya kuzingatiwa ni pamoja na kutafuta pembejeo za kisasa, kulima kwa kuzingatia teknolojia na kutafuta masoko kabla ya kuingia kwenye kilimo.

“Angalia utapata wapi pembejeo za kisasa kuanzia mbegu, viuatilifu, mbolea na dawa kwa kufanya haya kilimo chetu kinaweza kuboreshwa. Na kabla hujaanza kuzalisha pata taarifa ya masoko ujue aina gani ya bidhaa zinahitajika ndipo uanze kulima,” alisema.

Na kuhusu suala la uhifadhi wa mazao, Waziri Hasunga alisema kwamba Serikali imewekeza vya kutosha, “na mwaka huu tunajenga vihenga vya kisasa.”

Waziri Hasunga pia alisema kwamba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) itakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 500,000.

Waziri huyo pia alieleza kuwa Serikali imeanza kuwatambua wakulima kama taaluma nyingine ambako watawasajili na kuwapa vitambulisho bure.

Share.

About Author

Leave A Reply