Thursday, August 22

MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA: Siri ya kulima bustani kwa vizimba

0


Japo ufanisi katika kilimo unahusisha matumizi makubwa ya ardhi, wataalamu wanapendekeza matumizi madogo ya ardhi kwa kufuata kanuni za kilimo bora ili kupata mazao mengi zaidi.

Mbinu hii ndiyo anayoitumia Lucas Malembo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kilimo biashara ya Malembo Farm katika mazungumzo yake na MWANDISHI WETU ELIAS MSUYA.

Swali: Nini siri ya kuwekeza katika kilimo cha bustani ya vizimba?

Jibu: Kwa ujumla kilimo kinalipa tofauti na watu wengi wanavyodhani. Inategemea unalima cha aina gani. Mimi nimechagua kilimo hiki cha bustani za vizimba (green house) nikiwa na malengo ya kibiashara. Nimeshafanya tathmini ya kutosha ya masoko ndiyo maana nimewekeza mtaji wangu nikitegemea faida.

Tanzania tunayo fursa kubwa ya kufanya kilimo cha umwagiliaji, lakini eneo kubwa linalofaa kwa umwagiliaji halimwagiliwi. Tunaweza kuwekeza katika maeneo madogo kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji kama hivi na kupata mafanikio makubwa. Nawashauri vijana wenzangu kuingia kwenye kilimo kwa kufuata fursa za umwagiliaji na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Swali: Kilimo cha bustani za vizimba kikoje?

Jibu: Kuna aina nyingi za vizimba kutegemea na vifaa vinavyotumika. Wapo wanaotumia vyuma na nailoni au nyavu na wengine wanatumia mbao au miti. Mimi hapa nimetumia miti na nyavu maalumu.

Nyavu hizi zinasaidia kuzuia wadudu waharibifu kwa asilimia 99 wakati nyavu nilizoezekea zinasaidia kuzuia mionzi ya jua isiathiri mimea. Jua linahitajika kwenye mimea lakini lisiwe kali sana.

Kwenye matuta ya bustani tumeweka mbolea za mboji kisha tunafunika kwa nailoni ili kuzuia unyevunyevu usipotee. Katika kila tuta, kuna mipira kwa ajili ya kumwagilia mimea. Mpira umetobolewa matundu kwa kila mmea hivyo maji humwagika kwenye mmea husika kwa kipimo maalumu ili maji yasipotee bure.

Swali: Umepanda mazao gani na unatarajia kupata mavuno kiasi gani?

Jibu: Natumia vizimba viwili vyenye ukubwa wa mita 50 kwa 30. Bustani ya kwanza nimepanda nyanya miche 3,500 kwa umbali wa senitimita 60 kutoka mche hadi mche. Kama unavyoona kwenye bustani hii, miche hii sasa ina siku 75 na ninatarajia kuanza kuvuna ikiwa na siku 90. Natarajia kupata kilo moja katika kila mche kwa wiki moja na uvunaji utakuwa ukifanyika kwa miezi sita mfululizo. Kwa hiyo kila wiki nitakuwa nikipeleka kilo 3,500 za nyanya sokoni.

Kwenye bustani ya pili yenye ukubwa huohuo, nimepanda miche 8,000 ya pilipili za rangi ya kijani, njano na nyekundu. Nafasi kati ya mche ni sentimita 30 tu. Baada ya miezi mitatu nitakuwa nikivuna kilo moja ya pilipili kwa kila mche kwa wiki na uvunaji utakwenda kati ya miezi mitatu hadi minne.

Jibu: Soko lipo la kutosha, kwanza ndani ya nchi ninalenga kuuza kwenye supamaketi na vilevile ninalenga kuuza nje ya nchi kwa nchi kama Kenya na Afrika Kusini.

Masoko ya nje ya nchi ni makubwa, tatizo wakulima bado hatujaweza kuzalisha mazao ya kutosha masoko hayo. Kwa mfano, kuna wakati kampuni moja ya Malaysia ilikuwa ikitaka tani 78 za mapapai kila wiki, iliyakosa kwa sababu hakuna mkulima mwenye uwezo wa kuzalisha kiasi hicho ambacho kimsingi unatakiwa kuwa na hekta 1,000 za ardhi. Kwa hiyo, tatizo sio soko, bali uwezo wa kuzalisha.

Swali: Mtu atajiuliza atamudu vipi gharama za kutengeneza mradi wote huu?

Jibu: Siyo lazima utumie gharama kubwa unapoanza bustani kama hizi. Unaweza kuanza kutengeneza bustani bila kufunika kwa nyavu hizi na ukapata mafanikio. Unaweza kufanya bustani ndogo tu hata kwa gharama za Sh100,000 na ukapata mafanikio. Kisha ukaendelea kuongeza uwekezaji wa gharama kubwa zaidi ili kupata mafanikio zaidi.

Share.

About Author

Leave A Reply