Sunday, April 21

Mwana FA kwa Kagere humwambi kitu

0


By Olipa Assa

Dar es Salaam. Mwanamuziki Mwana FA amesema mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere ni mfano wa kuigwa kutokana na namna anavyothamini nafasi anayopewa na kocha wake Patrick Aussems na hata anapokosekana pengo lake litaonekana.

MwanaFA alistajabishwa na kasi na upambanaji aliouonyesha Kagere katika mchezo wao dhidi ya JS Saoura ya Algeria, Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kwamba hata mechi zinazoendelea watakuwa wana uhakika wa kuvuna mabao mengi kupitia mshambuliaji huyo.

Aliongeza kuwa katika mchezo huo si Kagere pekee ndiye alionyesha maajabu alimtaja Muivory Coast, Pascal Wawa na Emmanuel Okwi raia wa Uganda jinsi walivyotumia uwezo na uzoefu wao kuhakikisha Simba inaichapa JS Saoura mabao 3-0.

“Kazi yoyote inahitaji bidii na ndiyo matunda ya mabao tano anayomiliki Kagere kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, naamini ataandika rekodi yake yeye na wenzake wote ambao wamelibeba Taifa la Tanzania dhidi ya nchi wanazowania nazo taji hilo.

“Hii ndiyo Simba bhana! Cheki inavyoonyesha maajabu dhidi ya nchi nyingine, lazima wapinzani wao wanapokuja kucheza Uwanja wa Taifa wawe na nidhamu ya hali ya juu na si kujiamini kupita kiasi,” alisema.

Alisisitiza kwamba ushindi huo utawajengea kujiamini kwa mechi zilizopo mbele yao hata watakaporudi kwenye Ligi Kuu Bara watakuwa na morali waliyoipata kimataifa.

“Simba ina wachezaji wanaotumia akili nyingi na nguvu hiyo ni silaha tosha ya kuwafanya waweze kufanya lolote wakati wowote na michuano yoyote ile kwa maana ya kimataifa na taifa wakapata ushindi,” alisema Mwana FA.

Share.

About Author

Leave A Reply