Monday, March 25

Mwamuzi Suba, Tambwe gumzo Mbeya, Yanga yaua

0


By Godfrey Kahango

Mbeya. Sahau kuhusu mvua na tope lililojaa kwenye Uwanja wa Sokoine, mchezaji bora wa mechi kati ya Tanzania Prison na Yanga alikuwa mwamuzi Meshack Suba na mshambuliaji Amissi Tambwe aliyeingia akitokea benchi na kufunga mabao mawili.

Mwamuzi Suba aligeuka kituko katika mchezo huo baada ya kufanya makosa mengi katika mchezo huo akitoa kadi nyekundu mbili na penalti mbili, wakati Yanga ikitoka nyuma na kuichapa Prison kwa mabao 3-1.

Tangu mwanzo wa mchezo huo Mwamuzi Suba alionekana kushindwa kwenda na kasi ya mchezo baada ya kuinyima Yanga penalti mbili baada Ibrahimu Ajibu na Heritier Makambo kuangushwa kwenye eneo la 18 na mabeki wa Tanzania Prison.

Hata hivyo dakika 45, Mwamuzi Suba alizawadia Prisons penalti baada ya Andrew Vicent ‘Dante’ kumdondosha Jeremiah Juma aliyekuwa akijaribu kumpita beki huyo.

Penalti hiyo ilipigwa na wachezaji wa Yanga waliomzonga mwamuzi huyo kabla ya Vicent ‘Dante’ kumpiga kichwa mwamuzi Suba, lakini katika jambo la kushangaza alishindwa kutoka kadi nyekundu na badala yake akatoa kadi ya njano kwa Dante na Ajib kutokana na vurugu hizo.

Baada ya kadi hizo Yanga walikubali kupigwa kwa penalti hiyo ambayo Jumanne Elfadhilo alifunga bao la kuongoza kwa Prisons.

Wakati timu hizo zinakwenda mapumziko, Mwamuzi Suba alitolewa uwanjani chini ya ulinzi baada viongozi waliokuwepo eneo la mlango wa kuingilia vyumbani wachezaji na waamuzi walianzisha vurugu, walitaka kumpiga mwamuzi.

Kipindi cha pili wachezaji wa Yanga walirudi na hasira na kucheza kibabe huku mwamuzi Suba akionekana kushindwa kutoka kadi kutokana na ubabe wa wachezaji hao.

Katika dakika 50, Mrisho Ngasa alizua taflani baada ya kumpiga kichwa Hassan Kapalata, kitendo hicho kilisababisha wachezaji wa timu zote mbili kuingia katika vurugu hizo.

Kitendo cha Ngasa kumpiga kichwa Kapalata kilimkela nahodha Laurian Mpalile wa Prison aliyeamua kumpiga kichwa Ngasa mbele ya mwamuzi kabla kumsukuma na kumdondosha chini.

Katika vurugu hizo Makambo alikwenda katika eneo hilo na kumpiga ngumi mchezaji wa Prisons, lakini Mwamuzi Suba alifanikiwa kutoa kadi nyekundu kwa Ngasa na Mpalile.

Baada ya kadi hizo kila timu ilirudi mchezoni na Yanga ilifaidika kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Ajib kwa mkwaju wa penalti katika dakika 74.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alimtoa beki Juma Abdul na kumuingiza Amiss Tambwe ambaye katika mchezo huo alionyesha ubora wake wa kuzifumania nyavu.

Tambwe alifunga bao la pili kwa Yanga dakika 74, akiunganisha vizuri krosi ya Ajib kabla ya kupachika bao la tatu dakika 92, akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Prisons waliojichanganya na kuanguka na kumwacha Tambwe aliyekimbia na mpira na kupiga shuti lililompita kipa na kujaa wavuni.

Share.

About Author

Leave A Reply