Monday, August 19

Mtulia: Mwanaume wa Kinondoni hakimbii majukumu, Baba wanne atoe matunzo

0


By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mbunge wa CCM Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia amesema mwanaume aliyepata watoto wanne pacha, Fammy Suleiman anapaswa kuchukua jukumu la kutoa matunzo kwa watoto wake licha ya kumtaliki mkewe Radhia Solomon.

Pia ametoa onyo kwa ndugu wa mwanaume huyo kutoa lugha za kejeli na kashfa kupitia simu na ujumbe mfupi kwa mama wa watoto hao pacha na kwamba TCRA itatumika kuwabaini na vyombo vya dola vitafanya kazi yake ikiwa wataendelea kumsumbua.

Mtulia amesema hayo leo Jumapili Aprili 21 wakati alipokuwa akikabidhi msaada wa chakula na vitu mbalimbali kwa mama wa watoto hao.

“Hili jambo ambalo ndugu wa mume wanalifanya ni kudhoofisha afya ya huyu mama na hawa watoto, niseme tu kama unaona hauko katika nafasi ya kumsaidia Radhia (mama wa watoto) kaa kimya, inamuathiri kisaikolojia na hawa watoto wanaumia,” amesema Mtulia.

Hata hivyo amesema ofisi yake inalifuatilia jambo hilo, “Mtu halazimishwi ndoa ila akae akijua hili ni jukumu lake lazima atoe matunzo, tumefuatilia na kubaini anakaa Tandika, mwanaume wa Kinondoni hakimbii majukumu yake ya msingi.”

Mtulia amesema ameitembelea familia hiyo ikiwa ni salamu zake za sikukuu ya Pasaka, amepeleka zawadi ambazo ni kilo 25 za mchele, 25 za sembe, 10 za maharage, ndoo ya mafuta pamoja na fedha Sh50,000.

Kwa upande wake mama wa watoto hao, Radhia amesema changamoto kwake ni matunzo kwa watoto hao lakini kubwa kwa sasa ni makazi.

Share.

About Author

Leave A Reply