Thursday, August 22

Mtu wa Pwani: Ajibu awakumbuke Juma Kaseja, Tegete

0


By Charles Abel

Dar es Salaam.MWAKA 2003, jina la Juma Kaseja lilikuwa halikauki midomoni mwa mashabiki wa Simba na wadau wa mpira wa miguu hapa nchini.

Ni mwaka ambao aliiongoza Simba kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akisimama kwenye milingoti mitatu ya timu hiyo huku akiwa kijana mdogo ambaye kiumri hakuwa amevuka miaka 20.

Kaseja aliokoa mikwaju miwili ya Zamalek kule Cairo Misri na kuiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 3-2 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika matokeo ya mechi mbili za nyumbani na ugenini, lakini kabla ya kufika hatua hiyo, ndani ya dakika 90, kipa huyo alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa idadi kubwa ya mashambulizi ya ana kwa ana ambayo yangeweza kuzaa mabao na kuitupa nje Simba.

Hata hivyo miaka 10 baadaye, Kaseja aliondoka vibaya Simba ambayo iliamua kuachana naye baada ya kupewa tuhuma za utovu wa ambazo mmoja wa viongozi wa timu hiyo alizielekeza kwa kipa huyo, japo hazikuthibitishwa hadi sasa na imepelekea.

Pamoja na kuitumikia Simba kwa miaka 10 akiipa mafanikio makubwa, Kaseja amekuwa hapewi heshima stahiki ndani ya klabu hiyo kongwe nchini na hatizamwi kama mmoja wa mashujaa wa Simba kama ambavyo wenzake aliocheza nao kwenye kizazi chake Seleman Matola, Amri Said, Victor Costa na Boniface Pawasa.

Kiufupi, Kaseja aliitendea wema Simba, lakini mwisho wa siku walimuacha aende zake na sasa wala hawaoni haja ya kumtambua kama shujaa wao jambo ambalo alipaswa kufanyiwa.

Lakini kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka jinsi mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete alivyoamua kukacha kujiunga na klabu ya Dalkurd ya Sweden ambayo ilimpeleka nchini humo kumfanyia majaribio ya kujiunga nayo, ili aweze kuitumikia mara baada ya kuridhishwa na kiwango chake.

Wakati huo Tegete akiwa kwenye ubora wa hali ya juu wa kufumania nyavu, ilitajwa kuwa Dalkurd wakati wanajiandaa kumsainisha mkataba Tegete lakini katika hali ya kushangaza, mpango huo ulikufa rasmi baada ya Tegete kuamua kukatisha siku alizotakiwa kuwepo Sweden na kurejea nchini ili awahi mechi ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga ambayo hata hivyo Yanga ilipoteza kwa mabao 4-3.

Miaka kadhaa baadaye, Tegete aliachwa na Yanga na leo hii ameshaanza kusahaulika kwenye vitabu vya kumbukumbu vya klabu na mashabiki wa timu hiyo licha ya kujitolea kuitumikia timu hiyo kwa mapenzi na moyo wa dhati hadi kufikia hatua ya kukatisha majaribio ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Kama Kaseja na Tegete wangeamua kuachana na Simba na Yanga katika kipindi kile walichokuwa kwenye ubora wao, pengine leo hii wangekuwa mastaa wakubwa wa soka duniani lakini waliamua kuzitumikia kwa moyo mmoja ingawa baadaye ziliwageuka na kuwaacha kwenye mataa.

Hadithi hii ya Kaseja na Tegete inaweza kutumika kumkumbusha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ambaye leo hii ana ofa mezani kutoka klabu kubwa Afrika ya TP Mazembe ambayo inataka kumsajili kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga mwishoni mwa msimu huu.

Kabla ya ofa hiyo ya Mazembe, tayari kulikuwa na nia kwa Yanga kumuongezea mkataba wa kuitumikia timu yao lakini pia timu yake ya zamani, Simba nayo ipo kwenye mipango ya kuhakikisha inamnasa ili awe sehemu ya kikosi chake msimu ujao.

Ofa hizo zimekuja katika wakati sahihi ambao Ajibu amekuwa kwenye kiwango bora, akifunga mabao saba na kupiga pasi za mwisho 16 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi cha Yanga.

Baada ya Mazembe kuweka kiasi kinachotajwa kufikia Sh 53 milioni za Kitanzania kwa ajibu, ni wazi timu zetu hizi mbili kubwa Yanga na Simba zitaweka kiasi kikubwa zaidi ya hicho ili kumshawishi Ajibu aachane na Mazembe ili ajiunge nazo.

Ajibu anapaswa kukumbuka kuwa fedha hizo ambazo Simba na Yanga zitampa zinaweza kugeuka shubiri siku za usoni kama ilivyotokea kwa kaka zake waliopita tofauti na ile ya Mazembe kwani ataenda kwenye klabu inayojali na kuthamini wachezaji ambayo inaweza kumfanya apige hatua kubwa kisoka kama ilivyotokea kwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Ajibu anapaswa kufahamu kuwa mara kwa mara mwisho wa mchezaji kwenye klabu za Yanga na Simba umekuwa hauna taswira nzuri na wengi wamekuwa wakiondoka vibaya na ili kumsaidia zaidi, asome kisa kilichowakuta kaka zake Tegete na Kaseja.


Share.

About Author

Leave A Reply