Saturday, August 17

MTAA WA KATI : Ole, Emery kila mmoja ana jinamizi linalommaliza

0


By Said Pendeza

KUNA mambo mengi ya kuhadithia kuhusu Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu. Ni wazi kabisa kama Liverpool na Man City zingekuwa Chelsea, Man United, Arsenal au Tottenham nadhani hadi sasa hivi, bingwa angekuwa ameshapatikana.

Kwa ligi inavyoendelea, hakuna ubishi Man City na Liverpool ndizo timu zilizopo kwenye viwango vyao bora kabisa kwa sasa.

Ndio maana zinashinda karibu kila mechi. Shida ipo kwa timu hizo zinazoshindania nafasi ya kuwapo kwenye Top Four. Ngumu kuyatabiri matokeo ya Arsenal.

Ngumu kufanya hivyo pia kwa Man United, Chelsea na Spurs. Hazina uhakika wa kushinda na ilivyo ni kwamba ushindi wao itokee tu. Ni rahisi kutabiri matokeo ya Man City na Liverpool.

Pengine hata Wolves, lakini si vigogo hao wanne waliopo kwenye vita kali ya kushindania nafasi mbili zilizobaki kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwenye ligi, kila timu kwa sasa imebakiza mechi mbili.

Lakini, utamu wake unakuja sehemu moja tu, kuanzia kwenye timu namba moja hadi ya sita, kila moja itahitaji kushinda ili kuufanya msimamo uendelee kubaki kama ulivyo kwa sasa. Sare au kichapo kwa timu yoyote kwenye hiyo Top Six, basi itapinduapindua msimamo.

Kwa mfano, Chelsea na Arsenal zisikwae kwenye mechi ijayo tu kisha Man United ikashinda basi msimamo utabadilika sana.

Pale kwenye mbio za ubingwa, Liverpool wakipoteza mechi ijayo tu kisha Man City wakashinda, basi mbio za ubingwa zitakuwa zimemalizwa rasmi. Hivyo ndivyo Ligi Kuu England inavyotia kizunguzungu msimu huu.

Lakini, kizunguzungu kingine ni kuhusu kiwango cha Arsenal kwenye mechi za ugenini msimu huu. Hakika ni jinamizi baya linalomwaandama kocha Unai Emery.

Lakini, wakati Emery akiwaza namna ya kuondokana na jinamizi hilo la mechi za ugenini, mwanzake Ole Gunnar Solskjaer huko Man United anakabiliwa na jinamizi David De Gea.

Kipa huyo Mhispaniola amekuwa na makosa mengi sana siku za karibuni na kuigharimu timu.

Kuna kitu kinasumbua kichwa cha De Gea huku ikielezwa kwamba Ed Woodward amegoma kumpa mshahara anaotaka huku PSG wakimvuruga kwa kudai watampa mshahara anaotaka, Pauni 350,000 kwa wiki.

Jambo hilo linatosha kumvuruga De Gea na kushindwa kutuliza akili yake ndani ya uwanja na kuruhusu mabao ya kizembe sana.Hiyo ndiyo kesi ya Ole huko Man United.

Kwa Emery, shida ni mabeki wake wanapocheza ugenini. Wanaruhusu mabao kama wamerogwa. Mechi 18 ilizocheza ugenini kwenye ligi hadi sasa, Arsenal imeruhusu mabao 34, wakati yenyewe imefunga mabao 28 tu.

Mechi walizoshinda ni sita, sare nne na wamechapwa mara nane. Kwenye mechi zao za ugenini wamevuna pointi 22 tu, chache kuliko hata walizovuna Wolves, Leicester City, Crystal Palace na Watford kwenye mechi za ugenini. Hakika hilo ni eneo ambalo Emery anapaswa kuliboresha kwa msimu ujao kama anahitaji timu kufanya kweli na kuwa ya kiushindani kwenye ligi hiyo msimu ujao.

Mechi zao zilizobaki kwneye ligi msimu huu bado wana mchezo mmoja wa ugenini, bila ya shaka watahitaji kupata matokeo mazuri ili walau kuongeza idadi zao ya mechi walizoshinda ugenini.

Hayo ndio majinamizi yanayowakabili Ole na Emery. Laiti kama De Gea angekuwa na umakini kwenye mechi za karibuni kwenye hiyo vita yao ya kuwania Top Four basi mambo yasingekuwa mabaya Man United.

Na Emery kama Arsenal ingebadilika na kuwa bora ugenini, wasingekuwa kwenye wakati mgumu wa kuigusa Top Four kwa sasa.

De Gea ni kipa bora sana, lakini kwenye soka ili kushinda taji lolote unahitaji mtu imara golini. Uimara wa makipa Ederson na Alisson ndiyo wanaozifanya Liverpool na Man City vita yao kuwania ubingwa wa ligi kuendelea kuwa hadi pengine hadi mwisho wa msimu.

Share.

About Author

Leave A Reply