Wednesday, August 21

Msiba wa Mengi Wenye ulemavu wahemewa

0


By Bakari Kiango na Fortune Francis, Mwananchi

Maisha ya binadamu yana siri kubwa ndani yake, tangu kuzaliwa mpaka siku unaondoka duniani hakuna mtu huwa anafahamu lengo la kuletwa kwake duniani.

Unaweza kuzaliwa katika familia maskini ukadharauliwa na watu wengi, lakini mwishowe ukawa mtu mwenye msaada mkubwa hata kwa walio kudharau na ukawasaidia bila kukumbuka mabaya yao.

Wakati mwingine watu wanaweza wasikudharau lakini kwa sababu unajua shida ya kuishi katika kipato cha chini na kukosa baadhi ya mahitaji muhimu siku unapobarikiwa kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi ni lazima utaguswa kipekee na mahitaji ya watu wengine kwa kuwa unafahamu machungu wanayopitia. Hilo limedhihiri kwa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za Ipp, Reginald Mengi alivyoweza kutumia uwezo wake katika kuwasaidia watu wenye uhitaji maalumu ili kuhakikisha wanakuwa katika hali bora ndani ya jamii.

Mengi ambaye ni mfanyabishara maarufu alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, mwaka huu akiwa Dubai, Falme za Kiarabu alikokuwa akipatiwa matibabu na anayezikwa leo katika Kijiji cha Nkuu Sinde, Machame mkoani Kilimanjaro.

Licha ya kuwa kuondoka kwake kumegusa kila mtu lakini msiba huu uliwagusa kipekee watu wenye ulemavu kwa sababu huenda ile faraja waliyokuwa wakiipata, mitaji waliyokuwa wanapewa, ufadhili wa kimasomo na matibabu isiwepo tena na hata ikiwepo siyo kwa kiwango kile cha awali.

Akimzungumzia mfanyabiashara huyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Ummy Nderiananga anasema walipokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mengi.

“Tulipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo chake, alikuwa baba yetu mpendwa. Mengi ana historia ya karibu robo karne na watu wenye ulemavu.

Ameeleza hayo juzi wakati wa shughuli za kuaga mwili wa Mengi iliyoongozwa na Rais John Magufuli na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi waandamizi wa Serikali iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Anasema enzi za uhai wake, Mengi alijitoa kwa hali na mali kuendeleza utetezi kwa watu wenye ulemavu hasa kwenye sekta ya afya, michezo na elimu.

“Siku zote Mengi aliamini katika mambo mawili yaani utu na upendo kwa watu wenye ulemavu. Tumefadhaika sana na kifo chake tunaungana na familia na Watanzania kuombeleza,” anasema Nderiananga.

Akinukuu maneno ya Mengi Nderiananga anasema “ukimpenda mtu mwenye ulemavu utamheshimu na kuuthamin utu wake. Hakika alikuwa ni baba na rafiki,” anasema.

Nderiananga anasema Mengi hakusita kuonyesha hisia zake kwa watu wenye ulemavu na alitumia ushawishi wake kwa kuwaita marafiki zake ili kulikomboa kundi hilo. “Alikuwa na upendo mkubwa kwetu, ndio maana alianzisha taasisi ya watu wenye ulemavu. Taasisi hii ilikuja baada ya kila mwaka kukutana na Mengi kula chakula cha pamoja.

“Tukikutana katika hafla hiyo tunafurahi na kucheka na yeye alikuwa akiwaita marafiki zake na wanaotusaidia na kutuahidi mahitaji mbalimbali. Katika tafakuri tukaawambia Mengi mbona tunakula halafu tunaondoka tutafanyi nini? Anahoji Nderiananga.

Hata hivyo, Nderiananga anasema katika hafla iliyofanyika mwaka jana ambayo mgeni ramsi alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alimpa wazo Mengi la kuanzisha taasisi ya watu wenye ulemavu.

“Kwa kuwa Mengi alikuwa msikivu alikubaliana na ombi la Majaliwa na hatimaye alianzisha taasisi iliyozinduliwa mwaka jana,” anasema Nderiananga

Mbali na hilo, anasema katika kitabu chake Mengi cha I can, I will, I must, hakuwaacha nyuma wenye ulemavu kwa kuchapisha nakala maalumu kwa staili ya nukta nundu.

“Sijawahi kuona mwandishi akatumia fedha zake kuwakumbuka watu wenye ulemavu, tumepata pigo sana. Mei 2 kila mwaka itakuwa ni siku ya kutafakari na kuona namna ambavyo mchango wa Mengi umekuwa na manufaa kwetu,” anasema

Wakati anaeleza hayo, Rukia Khamisi anasema “Mzee Mengi nilikutana naye mwaka 1993 alipokuja Chuo cha ufundi Yombo kuzindua ujenzi wa sekondari ya watu wazima iliyobuniwa na walimu wakishirikiana na wananchi. Kipindi hicho nilikuwa nasomea usekretari.

“Katika hafla hiyo kulikuwa na nyimbo ngonjera, maigizo ambayo nilishiriki kikamilifu sanjari na kusoma risala kwa mgeni ramsi (Mengi) ambaye aliahidi kusaidia ujenzi wa sekondari na akafanya hivyo. Baada ya kumalizika kwa shughuli Mengi aliniambia niende ofisi kwake kesho yake,” anasema.

Rukia anasimulia kuwa baada ya kwenda ofisini kwa mfanyabiashara huyo, aliuliza kozi aliyokuwa akisoma (Rukia) chuoni hapo huku akimpongeza kwa ujasiri aliouonyesha wakati wa hafla hiyo.

“Aliniuliza nimesoma sekondari, nikwambia hapana je, ungependa kusoma nikamjibu ndiyo. Baada ya maelezo hayo Mengi aliniahidia kunilipia ada ya mwaka mzima na kunipa Sh5,000 ya matumizi kwa kila mwezi,” anasema Rukia.

Anasema taarifa za kifo chake zimemhuzunisha sana na kwamba kwa hatua aliyofikia ikiwamo kufanya kazi katika maeneo mbalimbali kumechangiwa na mfanyabiashara huyo.

“Sasa najivunia fani yangu ya usekretari lakini isingekuwa Mengi nisingefika hapa. Namshukuru sana kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia watu wa kada mbalimbali bila kujadili kabila, dini au rangi,” anasema Rukia akiwa na huzuni kubwa.

Naye Sylvester Joseph aliungana na Rukia kwa kusema enzi za uhai wake Mengi alikuwa ni hodari na mpenda maendeleo anayependa kusikiliza matatizo ya wananchi.

“Nilikutana na Mengi mwaka 2008 katika hospitali ya Muhimbili nilikokuwa nikipatiwa matibabu baada ya kupata ajali wilayani Tarime. Mengi alifika kuangalia wagonjwa lakini sikusita kumweleza shida yangu na akaahidi kunisaidia.

“Alinisaidia kwenye matibabu hadi leo hii nimepata ahueni licha ya kupata ulemavu namshukuru sana kwa moyo wake. Mengi ni mtu mwenye moyo wa tofauti aliyejishusha.

“Ukibahatitika kukutana na Mengi na kumweleza shida zako hasiti kukusaidia kutokana na upendo wa dhati aliokuwa nao wakati wote,” anasema.

Naye Bahati Hamidu anasema alimfahamu Mengi tangu mwaka 2013 baada ya kuelezwa na rafiki yake kuwa mfanyabiashara huyo ni mtu anayewasaidia watu mbalimbali.

Hamidu anasema baada ya kupewa taarifa alifanya jitihada za kufika ofisini kwa Mengi mara tatu bila mafanikio, lakini walipoalikwa kwenye chakula cha mchana katika ukumbi wa Diamond Jubilee akafanikiwa kuzungumza naye.

“Mengi aliniambia nimpelekee wazo langu la biashara. Siku iliyofuata nilienda ofisini na kumpa wazo, kisha alinikabidhi Sh300,000 zilizoniwezesha kuanzisha biashara ya kudarizi,” anasema Hamidu.

Kwa upande wake, Elias Kapingu ambaye ni dereva wa pikipiki ya magurudumu matatu anaeleza kuwa hatua aliyofikia bila ya Mengi asingeifikia.

Kwa mujibu wa Kapingu, chanzo cha kupata bajaji yake ni Mengi aliyemwezesha kwa kumuongezea kiasi cha fedha alizonunulia usafiri huo.

Kapingu anasema alipata taarifa kuwa kuna kampuni inakopesha pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama bajaji, lakini hakuwa na uwezo wa kukopa.

Anafafanua kuwa masharti ya kupata mkopo wa pikipiki hiyo ilikuwa ni lazima utoe kiasi cha fedha na alipomfuata Mengi hakusita kumsaidia.

“Kilichonishawishi kwenda kwa Mzee wangu Mengi kila tukikutana alichokuwa anatusisitiza ni kutokata tamaa na kuhakikisha tunajaribu,” anasema Kapingu.

Share.

About Author

Leave A Reply