Sunday, August 25

Mnyeti kuwachukulia hatua wanasiasa wanaopinga maendeleo

0


By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametoa onyo kali kwa wanasiasa wanane wa kata ya Kitwai wilayani Simanjiro wanaotuhumiwa kurudisha nyuma maendeleo kwa kukataza wanafunzi wasisome kwenye madarasa ya Shule ya Msingi Kitwai B yaliyojengwa na mdau wa maendeleo.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 24,2019 akizindua madarasa matatu mapya ya shule hiyo, Mnyeti amesema atawachukulia hatua kali wanasiasa wanaoshawishi wananchi kususia maendeleo.

“Hatutakubali kuona watu wachache wanapinga maendeleo, hivyo Serikali itamuunga mkono mdau huyo wa maendeleo Sanare Mollel ambaye pia ana mpango wa kumalizia majengo ya zahanati ya kijiji,” amesema Mnyeti.

Amesema wanasiasa hao wanampinga mdau huyo kwa sababu ni mfugaji mkubwa ambaye amefuata taratibu na kanuni zote za kuingia ndani ya kijiji hicho bila kuvunja sheria, kwani Mtanzania anaruhusiwa kuishi popote.

Amesema haiwezekani Mollel ajitolee kujenga madarasa matatu kisha baadhi ya wanasiasa wanawaambia wananchi wasisomeshe watoto.

Diwani wa kata hiyo, Nyika Shawishi amesema wapinzani wake wa kisiasa ndio wanaosababisha hali hiyo kwani wanaona maendeleo yakifanyika sifa zitakuwa kwake.

“Maboma matano yanayoongozwa na viongozi niliowashinda kwenye uchaguzi uliopita ndio wanasababisha uchochezi wa kugomea maendeleo,” amesema Shawishi.

Naye Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo, amesema shule hiyo imegharimu Sh47.3 milioni, mdau wa maendeleo alijitolea Sh30 milioni na nguvu za wananchi zimegharimu Sh12.3 milioni.

Tairo amesema jamii ya eneo hilo haioni elimu ni muhimu ndio sababu wanawasikiliza wanasiasa wachochezi wakatae maendeleo kutokana na ufinyu wa uelewa.

Share.

About Author

Leave A Reply