Wednesday, August 21

Mkwasa ataka Yanga ifumuliwe

0


By Imani Makongoro

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa amekiangalia kikosi cha Yanga na kumuuma sikio, Kocha Mwinyi Zahera akimtaka akifumue kikosi chake kama kweli anataka kurejesha taji la Ligi Kuu Bara ambalo kwa misimu miwili linashikiliwa na watani wao wa jadi, Simba.

Mkwasa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, alisema kuwepo kwa taarifa za kuondoka kwa mastraika wawili tegemeo wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu na Heritier Makambo kunamfanya Zahera afanye mpango ya kuvuta majembe ya maana ili kuepuka unyonge wa kuburuzwa na Simba waliotetea taji mapema na kuiachia Yanga nafasi ya pili.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga aliyetamba pia na timu ya taifa, alisema kuna haja ya kuimarisha kikosi hicho ili kiweze kuwa tishio zaidi msimu ujao.

Alisema timu hiyo inahitaji kuwa na nguvu za pembeni kwa kuongeza wachezaji wawili aina ya Simon Msuva ambao watakuwa na kazi ya kupeleka mipira mbele.

Kwa sasa Yanga inawategemea Mrisho Ngassa, Ibrahim Ajibu, Deus Kaseke na Godfrey Paul ‘Boxer’ katika winga zao, lakini wakishindwa kuonyesha makeke kama yale ya Msuva anayetamba kwa sasa katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco.

“Nafasi nyingine ambayo Yanga inapaswa kuiboresha ni kipa, waliopo wanapaswa kuongezewa nguvu kwani bado golini kunatetereka anahitajika kipa wa ushindani.

“Vilevile iongeze mabeki wawili ili kuimarisha safu yao ya ulinzi ambayo binafsi naiona inahitaji nguvu mpya,” alisema kocha huyo.


Share.

About Author

Leave A Reply