Thursday, February 21

Mjane anayesomesha mwanaye urubani kwa kuuza mkaa aanza kupokea matumaini

0


Dar es Salaam. Tangu habari za maisha yake zilipochapishwa kwa mara ya kwanza na Mwananchi, Bahati Masebu (41), mkazi wa Kunduchi jijini hapa anayemsomesha bintiye urubani kwa kuuza mkaa, ameendelea kuvuta hisia za watu wengi kutaka kujua maisha anayoishi.

Bahati anamsomesha urubani binti yake Nyamizi Ismail (20), kwa kuuza mkaa na wakati mwingine kuomba msaada misikitini na makanisani.

Hata hivyo, habari njema ni kwamba mama huyo ‘mpambanaji’ ameanza kupokea misaada ya fedha na ahadi ya ufadhili wa masomo ya bintiye kutoka kwa wasamaria wema.

Novemba 4, Mwananchi lilichapisha habari ya mjane huyo ikieleza namna alivyopambana kumsomesha bintiye hadi stashahada (diploma) ya urubani katika Chuo cha Aviation Tanzania University (Tauc) kilichopo Tabata kwa kuuza mkaa na kuomba misaada.

Chuo hicho kinatoa mafunzo ya awali ya ofisa na meneja uendeshaji wa ndege.

Bahati alifiwa na mumewe 2013 aliyepata ajali ya gari wakati akitoka kazini.

Katika mahojiano, mama huyo alisema alikuwa akilipa kati ya Sh6 milioni hadi Sh9 milioni kwa mwaka kwa ajili ya masomo ya Nyamizi, lakini sasa anahitajika kupata kati ya Sh80 milioni hadi 100 milioni za ada katika vyuo vya juu ili bintiye aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani.

“Nawashukuru sana Mwananchi, kuna watu wengi wameshanipigia simu ndani na nje ya nchi, wapo wanaonibeza na wengine kunipongeza, lakini wapo wanaonitumia fedha,” alisema Bahati jana.

Alisema yupo Mtanzania anayeishi nje ya nchi aliyempigia simu na kumwambia atamtumia fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Pia, alisema kuna mwingine anaishi Arusha ambaye amemtumia Sh100,000 na mwingine amemtumia Sh5,000 na mwingine Sh5,000. “Lakini wapo ambao wananipigia simu na kuniahidi kunisaidia fedha za ada na matumizi.”

Alisema mbali na hao, kuna Mtanzania mwingine anayeishi nje ameomba amtumie nakala ya vyeti vya Nyamizi vya chuo na sekondari, ili athibitishe maendeleo yake kabla hajatoa msaada wa ufadhili.

“Lakini baadhi yao wametushauri tufungue akaunti na Nyamizi ajiunge na mitandao ya kijamii kama WhatsApp waweze kuwasiliana nao kusudi wamsaidie hasa wale wanaoishi nje ya nchi. Kiukweli tunapokea simu nyingi, namshukuru Mungu,” alisema Bahati.

Akizungumzia ahadi na misaada aliyoanza kuipokea mama yake, Nyamizi aliwashukuru wote wanaojitolea na wanaoonyesha nia ya kumsaidia.

Aliwashauri wasichana wenzake wenye ndoto tofauti katika maisha yao waanze kwa kumweleza Mungu mahitaji yao kisha wairudie jamii inayowazunguka.

Share.

About Author

Leave A Reply