Saturday, August 24

Mivutano ya wazazi yawashindisha njaa wanafunzi

0


By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Handeni. Kutoaminiana baina ya wazazi kumesababisha wanafunzi wa shule ya Sekondari Kileleni Wilayani Handeni kukosa chakula cha mchana shuleni.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kileleni, Eliakim Kipele amesema leo Jumatano Mei 29, 2019 kuwa shule hiyo haitoi chakula cha mchana kwa sababu Sera ya Elimu inataka wazazi wenyewe waunde kamati na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Juma la Elimu linaloendeshwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Wilayani Handeni, Kipele amesema  wazazi wenyewe hawaaminiani jambo linalosababisha ugumu katika utoaji chakula shuleni.

“Wakati mwingine wazazi wanalazimisha kuleta hela kwa walimu, lakini Sera hairuhusu kwa hiyo hapo ndipo lilipo tatizo,” amesema Kipele.

Amesema mkakati uliopo kwa sasa ni kuwasaidia wazazi waunde kamati na waaminiane ili watoto waanze kupewa chakula shuleni.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo, wamesema wana uwezo wa kuchangia chakula lakini mpaka watakapopata uongozi wao.

Mmoja wa wazazi hao, Salim Hassana anasema kinachotokea sasa ni kila mzazi kumpelekea mtoto wake chakula.

“Kwa hiyo mtoto wako asipokula nyumbani na usipo mpa hela anashinda na njaa shuleni na hili ni tatizo letu, tutafanyia kazi maoni ya wadau kuhusu chakula,” amesema Hassan.

Mwenyekiti wa Juma la Elimu na Mshauri wa Elimu kutoka Shirika la Save The Children, James Sangoro amesema chakula ni jambo muhimu linalomfanya mtoto asome na kuelewa darasani.

“Ubongo unafanya kazi ukipata sukari inayotokana na wanga, kwa hiyo hatuwezi kuinua elimu kama watoto hawatapata chakula,” amesema Sangoro.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema utoaji wa chakula ni kati ya vipaumbele vilivyopo wilayani humo.

Gondwe amesema shule pia zina miradi ya mashamba ambayo pamoja na kuhakikisha uhakika wa chakula, inasaidia kuwajenga watoto kujitegemea.

Share.

About Author

Leave A Reply