Saturday, August 24

Miundombinu ya uhifadhi chakula iandaliwe

0


By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Kilimo Tanzania, Timothy Mmbaga amesema kabla ya kufanya uzalishaji wa mazao, ni vyema kuangalia miundombinu ya uhifadhi wa chakula iliyopo kama inaweza kukidhi kiasi kitakachozalishwa.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 23, 2019 katika Mjadala wa Nne wa Mwananchi Jukwaa la Fikra uliobeba mada ya ‘Kilimo, Maisha yetu’ unaofanyika katika ukumbi wa Kisenga Jijini Dar es Salaam.

Amesema kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki, wazalishaji wa bidhaa wamekuwa wakihakikisha kuwa kile wanachokizalisha kinatosha kuuzaa na si kwa ajili ya kutunza.

“Hata ukiangalia wale wanaolima bidhaa za matunda na mbogamboga hakuna ‘Cold Chain’ iliyoandaliwa kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao. Licha ya kuwa sehemu hiyo ina fursa kubwa lakini miundombinu ni changamoto kubwa.

“Endapo tutaweza kutengeneza miundombinu bora itakuwa ni fursa kwetu ya kuhifadhi chakula kingi ambacho kinaweza kufikia hata tani 500,000, hizi hata njaa ipige kwa miaka minne sisi tutakuwa hatuna wasiwasi na sekta binafsi mna nafasi kubwa ya kuwekeza katika upande huu,” amesema.

Amesema mbali na kutokuwepo kwa miundombinu bora ya kuhifadhi mazao, lakini hata ubora wa uzalishaji wa bidhaa za ndani umekuwa ukizingatia zaidi vigezo vya masoko ya nje kuliko ya  soko la ndani.

“Wapo wengi wanauza bidhaa zao katika masoko ya nje tena kwa kuzingatia vigezo vyote, kwa nini wanashindwa kufuata vigezo vinavyohitajika katika soko la ndani ili waweze kuziuzia hoteli zetu,” amehoji.

Share.

About Author

Leave A Reply