Thursday, February 21

Miaka miwili baada ya tetemeko Kagera aendelea kuishi hemani

0


Kabla ya tetemeko la ardhi la Septemba 10, mwaka 2016 mjini Bukoba maisha ya Sulaiya Selemani (69) hayakuwa magumu kama ilivyo sasa. Tangu wakati huo familia yake ya watu sita ilipoteza dira.

Aliishi kwenye nyumba ya bati yenye vyumba vinne iliyoezekwa vizuri na kuitosha familia yake. Walipata usingizi wa pono kwa kuwa hawakuwa na kero kupambana na mifereji ya maji ya mvua ndani ya nyumba kama ilivyo leo.

Miaka miwili baada ya tukio hilo lililoangamiza maisha ya watu 17 hakuna kilichoimarika tena zaidi ya mlezi huyu wa wajukuu kujipatia umaarufu mtaani kama bibi anayefanya kila aina ya kazi ya kibarua inayotokea mbele yake.

Huamka alfajiri kwa ajili ya kufanya vibarua mashambani, bustanini au kufua nguo za watoto na watu wazima kwenye familia zinazohitaji huduma yake. Kila ifikapo saa saba mchana ni lazima awe amerejea nyumbani kuwapikia wajukuu wake.

Haya ndiyo maisha yake ya kila siku. Ni mjane anayekaa mtaa wa Buyekera ambaye anabeba jukumu la kuwalea wajukuu wake baada ya wazazi wao wawili kufariki dunia na kuachwa wakiwa hawajafikia umri wa kuanza shule ya msingi.

Septemba 10, 2016 siku lilipotokea tetemeko alikuwa nyumbani na familia yake na ulikuwa wakati wa chakula cha mchana ambapo kishindo cha tetemeko kiliwafanya kutimua mbio na baada ya kurejea walikuta hakuna hata ukuta mmoja uliosimama katika nyumba yao.

‘’Ulikuwa ni muda wa kupata chakula cha mchana nikiwa na wajukuu wangu nyumba ilianguka yote Mungu alitusaidia hakuna aliyeumia au kujeruhiwa lakini tangu siku hiyo maisha yamekuwa magumu sana baada ya kukosa makazi ya kudumu,” anasema Sulaiya.

Pamoja na tukio hilo lililobadilisha mkondo wa maisha ni lazima familia yake iendelee kuishi ambapo pamoja na umri wake mkubwa analazimika kubeba majukumu yote ya kiongozi wa familia ambaye amebeba pia matarajio ya ndoto za wajukuu wake watatu.

Ni miongoni mwa wajane wanaopatikana kwenye kundi la wazee ambao badala ya kupumzika na kutegemea matunzo kutoka kwa watoto na wajukuu wao mambo huwa ni kinyume chake na kujikuta wao ndio wanategemewa kuendesha familia.

Kila siku anafanya kazi kwa wastani wa saa sita na malipo yake ni Sh1,500 na hii ndiyo sababu ya kukubali kila aina ya kazi pamoja na umri wake kutohimili tena kazi nzito ili aweze kupata mlo wa familia yake. Anasema anajua malipo anayopata ni kidogo lakini hawezi kuishinda hali hiyo kwa kuwa bado familia yake hususani wajukuu wake ambao huwa na matumaini kila anaporejea nyumbani kwa kuwa huonekana wana uhakika wa kupata mlo.

‘’Najua wananipunja kwenye malipo lakini ni lazima nirejee na kilo ya unga nyumbani. Naridhika na hiyo Sh1,500 kwa siku sina mjukuu anayesoma shule yupo aliyemaliza lakini hakubahatika kuendelea na masomo,” anasema.

Licha ya kushindwa kujimudu baada ya tetemeko, kikongwe huyo anashangaa mpango wa Kusaidia Kaya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kumpita pembeni tofauti na wengine wanaonufaika ambao anaona wana unafuu wa kuendesha maisha yao. Anasema kwa vibarua anavyofanya na kiasi kidogo anacholipwa hana uwezo wa kujiwekea akiba ya baadaye kwa kuwa fedha yote huishia kwenye matumizi ya kila siku.

Share.

About Author

Leave A Reply