Monday, August 26

Miaka 22 imepita Prince William na Harry bado wamlilia mama yao Princess Diana

0


London. Prince William na Prince Harry wamemkumbuka mama ya Princess Diana, ambapo William alisema, “Ni maumivu yasiyo kifani kuondokewa na mpendwa nawako” huku Harry akisema huzuni ya kumbuka mama yake ilimfanya atumbukie kwenye ulevi wa pombe na bangi.

“Ni maumivu yasiyo kifani” ndivyo alivyoanza kusema William alipokuwa akielezea namna anavyomkumbuka mama yake Princess Diana aliyefariki kwa ajali ya gari mwaka 1997 jijini Paris nchini Ufaransa.

Wakati Princess Diana anakufa William alikuwa na umri wa miaka 15 na mdogo wake Harry alikuwa na umri wa miaka 12.

Akihojiwa na BBC, William ambaye sasa ana umri wa miaka 37, alisema maumivu ya kufiwa na mama yake ni makubwa kwa sasa kiasi cha kumfanya hata kazi yake ya urubani wa helikopta za uokoaji aione ngumu.

“Naona kama kifo kipo mlangoni” ndivyo anasema William kwamba hali hiyo humkuta anapokuwa akirusha chopa.

Alisema, “kazi inanifanya niwe mnyonge, nijisikie vibaya hasa pale unapofikiria kuwa kifo kipo mlangoni popote ninapokwenda. Huo ni mzigo mzito kuubeba na kuuhisi.”

“Nadhani unapoondokewa na matumaini kwenye umri mdogo..unahisi maumivu yasiyo kifani. Na pale unapojua maisha yako yanapitia kwenye hatua ngumu hiyo inakuwa ni maumivu.”

Alisema unaweza kuona kukosa matumaini kwa mtu aliyeondokewa na mpendwa wake kwa kuangalia macho yake au namna anavyozungumza.

 Prince Harry wa Uingereza, ameeleza kuwa alitafuta ushauri nasaha miaka minne iliyopita kukabiliana na huzuni ya kumpoteza mama yake, Princess Diana.

Mwaka juzi mwanamfalme Harry alihojiwa na gazeti la The Telegraph la Uingereza akasema kumpoteza mama yake katika umri mdogo kulisababisha aishi maisha ya hovyo.

“Naweza kusema kuwa kumpoteza mama yangu nikiwa na miaka 12 na hivyo kuzima hisia zangu zote kwa takriban miaka 20, kumekuwa na madhara makubwa, si tu katika maisha yangu binafsi bali pia kazi yangu,” alisema kwenye mahojiano hayo.

Harry alisema alitafuta ushauri wa kitaalamu akiwa na miaka 28 baada ya kupitia miaka miwili ya vurugu.

“Sikujua nilikuwa na tatizo gani. Njia yangu ya kukabiliana nalo ilikuwa ni kukiweka kichwa changu kwenye mchanga. Kukataa kamwe kumfikiria mama yangu kwa sababu kwa nini hiyo isaidie? Itakufanya tu uwe na huzuni. Haiwezi kumrudisha tena,” alisema.

Princess Diana alijulikana kama princess wa watu, alifunga ndoa na Prince Charles kwenye harusi ya kifahari katika Kanisa la St Paul mjini London mwaka 1981. Alimzaa mwanae wa kwanza William mwaka 1982, na wa pili, Harry, 1984.

Harry alipata shida kukabiliana na macho ya vyombo vya habari. Miaka mitano baada ya kifo cha mama yake, akiwa na miaka 16, baba yake alimpeleka kwenye nyumba ya kutibu wenye uraibu wa kilevi baada ya kukiri kunywa sana pombe na kuvuta bangi.

Share.

About Author

Leave A Reply